Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI WA VYUO VIKUU WAONGOZA KWA KUTUKANA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII


Serikali imesema wanafunzi wa vyuo vikuu wanaongoza kutukana na kutumia lugha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii. 


Angalizo hilo limetolewa na naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha jana Jumamosi Machi 24, 2018 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Unilife Compus iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwenge na kuvikutanisha vyuo vikuu vyote vya mkoa huo. 


Amesema yapo mambo matatu ambayo yanachangia wanafunzi kutofanya vizuri, yakiwamo matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), anasa na starehe zilizopitiliza na kujiingiza kwenye siasa ambazo zinawanyima fursa ya kusoma vizuri.


“Serikali imebaini mambo yanayochangia kufifisha na kudidimiza jitihada za elimu tunayoitoa kuonekana bure. Kuna vitu ambavyo siyo vizuri vinaendelea katika vyuo vyetu, ndizo changamoto tunatakiwa kukabiliana nazo. Chuoni unaweza kutengeneza au kuharibu maisha yako,” amesema.


Naye mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema wanafunzi wengi hawataki kujifunza kwa kutumia muda vizuri kwa kusoma vitabu.


"Tunabaki kuwa waigaji wa dhana za wenzetu wa magharibi, hatutaki kujifunza vitu vipya bali vilevile vya wenzetu vinatumika hadi leo. Wasomi wa Tanzania tunajishusha kwa sababu ya kushindwa kuleta mawazo mapya kwenye sekta ya elimu na afya," amesema Mghwira.

Na Janeth Joseph, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com