Mwenyekiti wa kijiji cha Nsalala Sandeko Ndegeleja Machungo
Serikali ya kijiji cha Nsalala kata ya Nsalala Tarafa ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imetunga sheria ya kutokomeza ndoa za utotoni kwa kupiga marufuku kila mwananchi anayetaka kuoa ama kuozesha lazima atoe taarifa kwa uongozi wa kijiji hicho.
Sheria hiyo inamtaka kila mwananchi kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ndiyo apatiwe ridhaa ya kufunga pingu za maisha.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 30,2018 na mwenyekiti wa kijiji cha Nsalala Sandeko Ndegeleja Machungo wakati wa mdahalo kuhusu Ukatili wa Kijinsia ulioandaliwa na Shirika la Kivulini kwa ufadhili wa shirika la Oxfam
Alisema viongozi wa serikali hiyo ya kijiji mara baada ya kupata elimu ya ukatili wa kijinsia kupitia mashirika mbalimbali,likiwemo shirika la Kivulini waliona ni vyema wakatunga sheria ndogo katika kijiji hicho ya kuzuia wananchi kuoa ama kuozesha bila ya kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji.
"Ili kutokomeza ndoa za utotoni,sisi tumetunga sheria za kuhakikisha watoto hawaolewi,hivyo ukitaka kuozesha lazima utoe taarifa kisha tunajirdhisha kama huyo anayeolewa au kuoa anastahili,kama yuko chini ya umri wa miaka 18 basi tunachukua hatua",alisema Ndegeleja.
Alisema kijiji kilikubaliana kutunga sheria hiyo mwaka jana na wananchi wamekuwa wakifanya hivyo na tangu ianze kufanya kazi hakuna changamoto tena ya ndoa kwa watoto wala mimba kwa wanafunzi.
Kaimu Ofisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya Shinyanga Aisha Omari aliipongeza serikali ya kijiji hicho na kutoa wito kwa vijiji vingine kuiga kwani mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni yanahitaji nguvu ya pamoja.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Soma zaidi hapa>>SHIRIKA LA KIVULINI LAENDESHA MDAHALO KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA KWA WANA MABADILIKO SHINYANGA