JANA tuliona katika mitandao ya kijamii waraka wa viongozi wetu wa dini,ukizungumzia masuala mbali mbali ya nchi na mwelekeo wake huku sehemu kubwa ya waraka huo ukijikita katika kuikosoa serikali juu ya namna inavyoendeshwa.
Tunafahamu viongozi wa dini wana wajibu wa kiutumishi katika jamii huku wakilinda dhamira yao ya kuhakikisha umoja wa nchi yetu unabaki kuwa salama kwa namna yoyote ile.
Inapotokea mazingira yoyote ya viongozi wetu wa dini kushindwa kusimamia wajibu huo jamii inayoongozwa na viongozi hao inapaswa ijisimamie yenyewe na kuwakumbusha wajibu wao huo
Sisi Watetezi wa Rasiliamli wasio na mipaka (WARAMI) tunaamini kuwa moja wa wajibu wetu ni kuhakikisha Jamii inapatiwa haki hiyo pasipo upendeleo wa aina yoyote ule wa kiimani, kisiasa kanda au hata kiukabila
Kwa vyovyote vile tunaona ni sahihi kwa sasa nasi kupaza sauti yetu kwa jamii ili pamoja na viongozi wetu hawa wa dini wakiwemo maaskofu wa KKKT tuone ni namna gani bora ya kuishi katika jamii ambamo watu wake wamechanganyika kwa utofauti tofauti baina ya dini, kabila, jinsia, ufuasi wa kiitikadi na kadharika
Tunatumia nafasi hii kuwakumbusha viongozi wetu wa dini wajitafakari kwa umakini na kuanza kuchagua aina ya maneno ama kauli sambamba na njia wanazotumia ili kutokuleta taharuki kwa jamii hasa wakizingatia ukweli kwamba mara nyingi sio kila maoni wanayoona wao yanafaa basi kwetu sisi waumini wao pia yanafaa kwa maana tuyafuate kama yalivyo.
Miongoni mwa masuala yaliyoandikwa katika waraka ule wa maaskofu wetu ni malalamiko kuhusu Katiba Mpya, Uhuru wa kutoa maoni, Usawa katika elimu, mauaji ya watu, uchumi Demokrasi, kodi kwa wafanyabiashara na ajira kwa vijana kwa kuyataja kwa uchache.
WARAMI, tunashangaa ni kwanini waraka huu wa salamu za PASAKA haukujikita zaidi katika kuwasisitiza waumini wake kujikita katika kuabudu, kumnyenyekea Mungu, kusoma bibilia na maandiko mengine ya dini na badala yake wakajikita katika maoni yanayong’ata na kupuliza
Watanzania wote ni mashahidi kuwa kwa sasa nchi yetu imejitanabaisha katika kutatua changamoto zilizokuwa zinaimbwa kila siku na wanasiasa hasa wa upinzani na kwa kweli tumeanza kuyaona matunda ya serikali kujikita katika kutatua changamoto hizo
Sote ni mashahidi kuwa Kuilazimisha Serikali kuitisha mchakato upya wa katiba ni jambo ambalo haliingii akilini kwa sasa kutokana na ukweli kwamba ni wanasiasa wenyewe hususan wa vyama vya upinzani ndio waliosusia na kukwamisha mchakato wa katiba kwa kutaka kulazimisha mawazo yao yawe bila kuzingatia msingi mama wa Demokrasia kuwa wachache wanasikilizwa wengi wanashinda.
Maaskofu wetu wamekazana kulalama kuhusu katiba mpya huku waumini wake wanaotuongoza hawana ufahamu kuhusu BIBILIA
Aidha, tumeona hivi karibuni namna Rais wa nchi alivyozungumza na jumuiya ya wafanyabiashara na kuweka wazi changamoto zote zinazowakabili wafanyabiashara ikiwemo suala la kodi na kuweka mkakati wa pamoja kulitatua, sasa kuendelea kulalamika kwenye hili hakuna tofauti na nongwa kwa kuwa hata muda alioutoa Rais kwa watendaji wake haujakwisha.
Maaskofu wetu wamezungumzia kuhusu utekwaji na mauaji ikiwemo utiaji wa hofu lakini hawajajikita kuelezea kwa kina hasa ni yepi?,
Sisi tunafahamu kuwa wapo watu walioathirika moja kwa moja na matukio ya kutekwa na kuteswa kwa vijana kama Mussa tesha wa Igunga, Joseph yona wa Temeke, Halidi Kagenzi wa CHADEMA na wengineo yalipaswa kukemewa tangu siku ya kwanza ya kutokea kwake na si kuyasubiri mpaka leo.
Tunawashangaa maaskofu wetu hawa kusema kuhusu usawa wa elimu huku wakifahamu kuwa wanamiliki chuo kikuu ambacho hivi karibuni kilipandisha ada ya masomo na Askofu mkuu alipoombwa kushusha ada akamwamuru mlinzi afungue geti na anayetaka alipe asome asiyetaka mlango uko wazi atoke, nafikiri Usawa wa elimu ulipaswa kuanza katika chuo kinachomilikiwa na KKKT na si vinginevyo.
Maaskofu wetu wanajaribu kutuaminisha kwamba wao ni wasafi na kila wanachozungumza ni sahihi je wanadhani wapo wasafi kiasi cha kuwa tayari kuchunguzwa na kuwekwa hadharani kuhusu Uhalali wa makanisa yao?.
Je maaskofu wetu hawa ni wasafi kiasi cha kuwa tayari kuchunguzwa matumizi ya mabilioni ya sadaka wanayokusanya kila siku?.
Ama maaskofu hawa wanaweza kuueleza umma kuhusiana matumizi ya misaada, misamaha ya kodi wanayopaswa kulipa na matumizi ya kodi hizo walizosamehewa na serikali.
MAASKOFU WETU WANATUMIKA?
Hatutaki kuamini kwamba viongozi wetu hawa wanatumika na wanasiasa kwa maslahi yao ama ya wanasiasa lakini nafikiri tunapaswa kufikiri sawa kwenye hili kwa kujijibu maswali machache yafuatayo?
- Ikiwa waraka huu wa Maaskofu wetu umesainiwa tarehe 15-03-2018, kwanini umetoka leo na si kipindi ulipoandaliwa ama siku ya ibada kama inavyokuwa kawaida ya siku nyingine?
- Kwanini waraka huu umetolewa siku moja baada ya waraka wa Mwenyekiti wa CHADEMA Mheshimiwa Freeman Mbowe ambao kimsingi maudhui yanafanana kiasi cha kutia shaka kuwa umeandaliwa na mtu mmoja na maaskofu kushirikishwa kuweka majina yao tu?
- Kwanini waraka huu wa Maaskofu umesambazwa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa CHADEMA ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu wa chama hicho mheshimiwa LEMA ambaye ndiye aliusambaza Waraka wa Mbowe katika muda unaofanana na njia zinazofanana?.
Ukijijibu maswali hayo hapo juu unaweza kupata picha halisi
WITO
- Tunatoa wito kwa Maaskofu wetu kujikita katika masuala mahsusi yanayohusu Dini, watuelimishe kwenye dini, wamuachie Kaisari yaliyo yake nay a Mungu yaliyo yake
- Tunawaomba maaskofu wetu wachague njia sahihi ya kupita kama walivyofanya wenzao waliowatangulia. Wapo viongozi wa dini walipoona wana wito wa kushiriki Siasa waliamua kuachana Upadri na Uaskofu na kujikita kwenye siasa
Social Plugin