Msanii
wa filamu, Wastara Juma amerejea nchini leo akitokea Mumbay nchini
India alikokuwa anapatiwa matibabu ya mgongo na mguu na kuwashukuru
Watanzania kwa namna walivyojitokeza kumchangia fedha za matibabu,
ingawa hazikutosha na kulazimika kuuza baadhi ya mali zake.
Akizungumza
leo Machi 1, 2018 nyumbani kwake Tabata ikiwa ni saa chache baada ya
kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, amesema
baada ya kufika hospitali alikutwa na matatizo mengine zaidi ya
aliyokuwa nayo jambo lililosababisha gharama za matibabu kuwa kubwa.
Wastara
alifanikiwa kwenda kwenye matibabu hayo, Februari 3, 2018 baada ya
kupata michango kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli
aliyemchangia Sh15 milioni.
Amebainisha
kuwa matatizo aliyokutwa nayo ni pamoja na uvimbe chini ya kalio na
kwamba, ndilo lilikuwa sababu ya kukaukiwa damu pamoja na kubainika kuwa
na uvimbe kichwani uliotokana na kupata ajali zaidi ya mara tatu.
“Kutokana
na matatizo haya ilifika mahali pesa nilizokwenda nazo ziliniishia na
kulazimika kuwaomba ndugu zangu wauze baadhi ya mali zangu, ikiwemo
kamera ili niweze kuendelea na matibabu,” amesema.
“Mtu
umeshafika kwenye matibabu tena nchi za watu unafanyaje? Kurudi bila
kutibiwa huwezi. Nililazimika kuwasiliana na ndugu zangu ili wauze
baadhi ya vitu vyangu niweze kutibiwa maana afya yangu ni muhimu kuliko
kamera.”