Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ACHUNWA NGOZI YA UUME..WACHUNAJI WAONDOKA NAYO KAHAMA


Mkazi mmoja wa kijiji na kata ya Kinaga, Kahama mkoani Shinyanga amechunwa ngozi ya sehemu za siri baada ya kuleweshwa kwa pombe.

Watu waliomchuna mkazi huyo anayejulikana kwa jina la Paschal Misana, wametoweka na hadi sasa hawajajulikana.

Diwani wa kata hiyo, Mary Manyambo alisema tukio hilo lilitokea Aprili 16, baada ya Misana kupigiwa simu na mtu aliyekuwa akimdai Sh200,000.

“Lakini kwa maelezo ya muathirika ni kuwa baada ya kufika nyumbani kwa mtu huyo alinyweshwa pombe hadi akapoteza fahamu na alizinduka asubuhi ya siku iliyofuata, akajikuta amechunwa uume wake kuanzia kwenye korodani,” alisema Manyambo.

Mganga wa zamu katika Hospitali ya Mji wa Kahama, Dk Abdallah Simba alisema jana kuwa mtu huyo alifikishwa hapo juzi mchana akiwa na hali mbaya.

“Aliletwa hapa sehemu yake ya uume ilikuwa imekatwa kwa kuzunguka na kisha kunyofolewa ngozi yote ya sehemu hizo hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi,” alisema.

“Wachunaji hao walimkata kitaalamu kwani hawakufika kwenye mishipa ya sehemu za siri na hivyo tayari ameshonwa na kurudishiwa alipokuwa amekatwa wakati wa kuchunwa.

“Sehemu zake za siri zinaweza kuendelea kufanya kazi kama kawaida kwa sababu sehemu za mishipa hazikukatwa.”

Akizungumzia tukio hilo akiwa hospitalini hapo anapoendelea na matibabu, Misana alisema baada ya kupigiwa simu hiyo alikwenda kwa lengo la kulipwa fedha alizokuwa amemkopesha mtu huyo.

“Nilimkopesha ng’ombe mmoja kwa thamani ya Sh200,000 na nilipofika baiskeli yangu iliingizwa chumbani na kisha nikakaribishwa ndani,” alisema.

Misana alisema baada ya kukaa, aliwaona wageni watatu waliokuwa chumbani, wawili wakiwa wanawake.

Alisema baadaye alitengewa ugali ambao alikula na wenyeji na baada ya kumaliza alipewa pombe aina ya shujaa waliyokuwa wakipewa pia wageni wengine.

Majeruhi huyo alisema baada ya kunywa pombe hiyo alipoteza fahamu mpaka asubuhi alipozinduliwa na mke wa mtuhumiwa.

Hata hivyo, alisema alishangazwa na kitendo cha kuwa peke yake akiwa uchi, huku akitokwa damu na sehemu zake za siri zikiuma.

“Sikujua chochote, baada ya watu kujaa wasamaria wema na kuanza kunipa huduma ya kwanza, walinieleza kuwa sehemu zangu za siri zilikuwa zimekatwa, hali iliyonishtua na baadaye polisi walifika wakanichukua na kunipeleka hospitalini,” alisema.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Simon Haule alisema tayari wanamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano.

Baada ya kuhojiwa, mtuhumiwa huyo alisema wageni wake watatu walihusika kumchuna ngozi Misana na kutoweka nayo na mpaka alipokamatwa hajui walielekea wapi.

Polisi wanaendelea kuwasaka wageni hao huku mtuhumiwa akiendelea kusaidia upelelezi.

Na Shija Felician, Mwananchi



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com