MMILIKI wa lori Mitsubishi Fuso lililogongana na basi la City Boys katikati ya wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 12 hapa wilayani Igunga mkoani Tabora, amekamatwa na polisi mkoani Ruvuma.
Katika ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Makomelo baada ya magari hayo mawili kuvaana uso kwa uso watu 46 walijeruhiwa pia chanzo kikidhaniwa kuwa mwendokasi wa lori.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wilbroad Mutafungwa alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa uchunguzi wa ajali hiyo umeanza.
Alisema katika uchunguzi huo, mmiliki wa Fuso hilo alipatikana mkoani Ruvuma na kwamba jitihada za kumsafirisha zilikuwa zikiendelea.
Kamanda Mutafungwa alisema aidha polisi inamsaka dereva na utingo wa Fuso hilo ambao baada ya ajali hiyo walikimbilia kusikojulikana.
Aliahidi kuwasaka usiku na mchana na kuhakikisha wanapatikana popote walipo.
Kamanda huyo aliwakumbusha madereva wote umuhimu wa kuendelea kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo na ulazima kwani ajali zinapoteza nguvu kazi ya taifa.
Kufuatia ajali hiyo, serikali tayari lishaagiza dereva atakayekematwa kwa kosa la kuendesha kwa mwendokasi apelekwe mahabusu na kisha mahakamani, kuanzia Alhamisi iliyopita.
Agizo hilo lilitolewa bungeni Dodoma siku hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akitoa taarifa ya ajali hiyo.
Aidha, Rais John Magufuli alilitaka Jeshi la Polisi, na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kujitathmini na kutafuta majawabu ya ajali katika salamu zake za rambirambi kufuatia ajali hiyo.
Basi la City Boys lilikuwa likitoka Karagwe mkoani Kagera kwenda Dar es Salaam kabla ya kugongana na Fuso lililokuwa linatoka Singida kwenda Igunga.
Katika taarifa yake, Waziri Mwigulu aliliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linamkamata na kumpiga faini dereva yeyote atakayeonekana anaendesha gari kwa mwendokasi na asiachiwe hadi atakapofikishwa mahakamani.
Alisema mahakama ikijiridhisha kuwa ni kawaida ya dereva huyo kuendesha kwa mwendokasi, anyang’anywe leseni.
“Pia nasisitiza kila basi la abiria liwe na madereva wawili ili mmoja akikamatwa mwingine aendelee na safari,” alisema Mwigulu.
Waziri huyo alilazimika kutoa kauli ya serikali bungeni baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa anaongoza kikao cha mchana, kuitaka serikali itoe ufafanuzi kuhusu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga kuhusu ajali hiyo.
Mbunge huyo wa CCM alidai ajali hiyo imetokana na ubovu wa barabara na kuitaka serikali iwe inatoza faini kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) pale ajali zinaposababishwa na ubovu wa miundombinu kama ambavyo Jeshi la Polisi linafanya kwa madereva wanaobainika kufanya uzembe barabarani.
Mlinga alisema ajali ilisababishwa na shimo barabarani, hivyo ipo haja Tanroads watozwe faini kwa kuwa wao pia wamekuwa wakitoza watu faini, "wakati mwingine bila sababu".
Katika taarifa yake, Waziri Mwigulu alikiri kuwapo kwa mashimo barabarani kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo lakini akasisitiza chanzo chake hakikuwa mashimo bali mwendokasi wa dereva wa lori.
"Dereva alikuwa anaendesha kwa kasi, alipokutana na lile shimo akaligonga lile basi. Yale mashimo yaliyopo pale si ya kutisha na kutwa nzima magari yaliyopita kwa mwendo wa kawaida hayakupata ajali," alisema.
Alisema serikali imekuwa ikiwatoza faini madereva wanaofanya makosa barabarani na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ajali lakini sasa makosa ya kuendesha kwa mwendokasi yamerejea tena na yanagharimu maisha ya watu.
"Naelekeza Jeshi la Polisi popote pale watakaposhuhudia dereva anakwenda kasi akamatwe, alipe faini na kuwekwa ndani kisha afikishwe mahakamani; na ikibainika ana rekodi ya makosa afutiwe leseni," alisema.