ALIYEZAA NA MCHINA KISHA KUIBUKIA KWA MAKONDA AZUA GUMZO MTANDAONI

Kambi ya siku tano inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwatafuta wanaume waliotelekeza watoto wao imempa umaarufu mitandaoni msichana aliyejitambulisha kwa jina moja la Safina.


Picha za msichana huyo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu alipoonekana nje ya ofisi za Mkuu wa Mkoa juzi asubuhi akiwa na mtoto wake anayefanana na Mchina.


Mwanamke huyo alipigwa picha akiwa amekaa kwenye ofisi hizo na mtoto wake huyo akisubiri foleni ya kupata msaada kutoka kwa wanasheria, maofisa ustawi wa jamii na polisi kutoka Dawati la Jinsia.


Baada ya picha hiyo kusambaa iliibuka mijadala kwenye mitandao hiyo wengi wakihoji kama kweli baba wa mtoto huyo atakuwa Mtanzania.


Baada ya muda kupita, ujumbe wa video iliyomrekodi msichana huyo ulisambaa akielezea alivyokutana na Mchina huyo na kuanzisha uhusiano ambao hatimaye ulisababisha kupatikana kwa mtoto huyo.


Kwenye ujumbe huo, msichana huyo alisema alikutana kwa mara ya kwanza na mchina huyo mwaka 2013 alipokuwa akifanyakazi kwenye kampuni ya ujenzi ya Hainan kutoka China.


Alisema wakati huo kampuni hiyo ilikuwa ikijenga majengo maeneo ya Gongolamboto jijini Dar es salaam na baadaye walihamia mkoani Dodoma na kuendelea na maisha.


"Nilikaa na baba yake huyu mtoto miaka mitatu mkoani Dodoma hadi alipopata matatizo na kuamua kurudi kwao China.... aliniambia atarudi na atanitafuta kwa njia ya simu lakini hadi leo sina mawasiliano naye," alisema.


Safina alisema anamlea mtoto huyo katika mazingira magumu bila msaada kwa kuwa mtoto huyo hana ndugu yeyote wa upande wa baba hapa nchini.


Safina alikuwa akizungumza huku akionyesha picha mbalimbali zinazoonyesha hatua za mahusiano yao, ikiwemo inayomwonyesha mzazi mwenzake akiwa amembeba mtoto huyo alipokuwa mchanga huko mkoani Dodoma.


Pia alikuwa akiwaonyesha waandishi wa habari vibali vya muda vya ukaazi alivyokuwa akitumia raia huyo wa China alipokuwa akifanyakazi nchini ambavyo vimeisha muda wake.


Msichana mwingine ambaye ujumbe wake wa video umesambaa ni Mwajuma Mohamed ambaye alisema kuwa ametelekezwa na mzazi mwenzake hivyo utaratibu ulioanzishwa na Mkuu wa Mkoa ni ukombozi kwao.


Alisema kwa sasa maisha ni magumu na kwamba ingawa yuko hai lakini anashindwa kuyamudu na kuhoji kuwa itakuwaje kama ikitokea akafariki na kumwacha mtoto wake bila baba.


Anahofu anaweza kuwa mtoto wa mitaani, alisema zaidi.


"Nawaambia wanaume huko waliko waache kutubebesha mimba na kututelekeza, huyu mtoto sijazaa na mzazi wangu nimezaa na wewe mwanaume uliyenikimbia, yaani nina dukuduku natamani nimkamate huyo mwanaume nimkamue ili aone uchungu wa maisha," alisema Mwajuma.


Awali, kambi hiyo ilipangwa kufanyika kwa siku tatu lakini kutokana na wingi wa wanawake waliojitokeza Makonda alitangaza iendelee kwa siku tano mfululizo ili kuhudumia wengi zaidi.


Wanawake hao wanapewa msaada wa kisheria na wanasheria mbalimbali, polisi na maofisa wa ustawi wa ajamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post