Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Phares Phinehas Chogelo (29) mkazi wa Old Shinyanga anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa kusababisha vifo vya watu wawili na kuwavunja miguu wengine wawili baada ya kuwagonga kwa gari.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule,tukio hilo limetokea jana Aprili 8,2018 majira ya saa tano asubuhi katika eneo la Ibinzamata barabara itokayo Shinyanga kuelekea Tinde.
Ameeleza kuwa gari lenye namba za usajili T. 105 DGQ Subaru Forester likiendeshwa na Phares Phinehas Chogelo (29) askari wa JWTZ, mkazi wa Old Shinyanga liliigonga pikipiki yenye namba za usajili T. 974 BSL aina ya San Lag iliyokuwa ikiendeshwa na Yahya Nasoro (36) mkazi wa Kitangili aliyekuwa amempakia Catherine Mwigulu (35) mkazi wa Nhelegani na kuwasababishia kuvunjika miguu yao ya upande wa kulia.
Ameongeza kuwa askari huyo pia alimgonga mpanda baiskeli ‘daladala’ Steven Joseph (25), mkazi wa Isela ambaye alikuwa amempakia abiria Nemem Joseph (26) mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Kolandoto, mkazi wa Butiama Mara na kuwasababishia vifo vyao wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Kamanda Haule amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari husika na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na vielelezo vipo kituoni.
Na Kadama Malunde – Malunde1 blog
Social Plugin