ASKOFU GWAJIMA AANZA KUAMSHA....ASIMULIA KISA CHA MWANAMKE

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ameeleza namna alivyonyang’anywa samani na muumini wake siku chache baada ya kumkabidhi.


Akitoa mahubiri katika ibada jana Aprili 15,2018 kanisani kwake, Ubungo jijini Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema aliamua kumrudishia muumini huyo na kukubali kuaibika.


Akisimulia kisa hicho mbele ya mamia ya waumini, Askofu Gwajima alisema wakati anaanza maisha na kazi ya kuendesha kanisa hilo, alipanga chumba kimoja katika eneo la Ubungo Msewe.


“Katika chumba nilichokuwa nimepanga kitu cha thamani nilichokuwa nacho ilikuwa ni carpet (zuria) la plastiki,” alisema.


Alisema wakati akiendelea kuishi katika chumba hicho, alitembelewa na muumini wake aliyemtaja kwa jina moja la Ester.


“Ester baada ya kuona mazingira ya chumba kile, akaniambia mchungaji hapa panahitajika stuli kwa ajili ya kukalia, nitazileta,” alisema.


Askofu Gwajima alisema kweli muumini huyo alimpelekea stuli nne na yeye akamshukuru kwa msaada huo.


“Baadaye muumini huyo akawa anatamba kanisani akiwaeleza waumini wenzake kwamba stuli zilizoko kwa mchungaji zimepelekwa na yeye,” alisema.


Gwajima alisema muumini huyo akawa anataka waumini wenzake wathamini mchango ambao anautoa kwa mchungaji.


“Baada ya kusikia hilo tulimwita na kumuonya asiwatishe waumini kwa kutumia kigezo cha msaada huo,” alisema.


Aliongeza, “siku moja nilitembelewa na ndugu zangu akiwemo mjomba, wakakaa kwenye stuli zile. baada ya muda mfupi Ester akaingia na kudai stuli zake mbele ya ndugu zangu.”


“Nikamtoa nje ili tuzungumze lakini msimamo wake ukawa uleule apewe stuli zake, ndugu zangu wakawa wanashangaa hawaamini kinachotokea,” alisema.


“Mjomba wangu akanieleza kwamba ina maana Gwajima huna hata stuli kwenye chumba chako.


“Nikamwambia stuli hizo si mali yangu ni za muumini hivyo nikawataka wageni wale wakae kwenye zuria, nikampa stuli zake.”


Amewataka waumini hao wasiogope kuaibishwa na mtu kwa sababu hatima ya maisha yao ipo palepale.


“Ni kweli niliaibishwa mbele ya ndugu zangu lakini sikukata tamaa na hatima ya maisha yangu ilikuwa palepale kama mnavyoniona leo,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post