Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKOFU KAKOBE : SITIKISIKI...HATA WAFANYE NINI,MIMI SIYO NYASI ZINAZOTIKISWA NA UPEPO

Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe amesema yeye siyo unyasi unaotikiswa na upepo.Amesema hata kama yeye na kanisa lake watapitishwa kwenye magumu, atashinda zaidi.

Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa inatokana na wito wa Idara ya Uhamiaji, ambako ametakiwa kwenda kuhojiwa leo.

Askofu Kakobe akiwahubiria waumini wake jana katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika kanisani kwake, aliwataka waumini hao kutoishi maisha ya unyasi yanayotikiswa na upepo bali wasimame imara kila wakutanapo na changamoto.

Kiongozi huyo ambaye leo anatarajiwa kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuandikiwa barua ya wito Aprili 5, ikimtaka afike katika ofisi hiyo saa 4:00 asubuhi, alisema hata wafanye nini atasimama imara kwa sababu wokovu wake siyo wa dhahabu bandia.

“Hata wafanye nini, mimi siyo nyasi zinazotikiswa na upepo... katika hayo yote nitashinda zaidi ya ushindi. Kanisa langu siyo la kuombea watu na kuwaponya magonjwa, hili ni kanisa ambalo hata likipita kwenye magumu kama Ayubu na Lazaro halitikisiki,” alisema.

Pia, Askofu Kakobe aliwataka waumini wake wasiyumbishwe na changamoto zinazojiinua katika maisha yao kwa lengo la kuharibu uhusiano wao na Mungu.

Akitolea mfano wa mtumishi wa Mungu, Lazaro na Ayubu namna walivyopitishwa kwenye majaribu, alisema kuna maisha ya binadamu ambayo watu wa Mungu wanapitishwa kwenye mambo magumu ili kupima imani zao.

“Shetani anamuogopa mtu anayemcha Mungu, hufanya kila njia ili kumuyumbisha aachane na Mungu. Tunapopita katika magumu, tuige mfano wa Ayubu ambaye mbali na kuyumbishwa na shetani alisimama imara katika imani, tuige imani hii,” alisema.

Askofu Kakobe aliwaambia waumini wake kuwa wasiwe walokole ambao wakitikiswa kidogo wanayumba, bali wawe imara kupambana na mawakala wa shetani wanaojiinua ili kufifisha Kanisa la Mungu.

“Tusiwe watu ambao hatuwezi kusimama katika imani eti kwa sababu hatuna mali. Mali zetu zimeondoshwa lazima tupite katika moto ili tuwe dhahabu mbele za Mungu,” alisema.

Alisema hakuna mamlaka wala utawala wowote utakaoweza kuwatenga na Kristo kama watasimama imara katika imani na kuwataka wasiwe dhahabu bandia.

Askofu Kakombe mbali na kuitwa uhamiaji, amekuwa kwenye misukosuko baada ya kutamka kuwa ana utajiri mkubwa kuliko Serikali.

Kufuatia kauli hiyo wakati wa mkesha wa sikukuu ya Krismasi Desemba mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianza kumchunguza juu ya uhalali wa utajiri wake na akaunti zake na watoto wake na kubaini kuwa fedha zilizopo zinatokana na michango, zaka na sadaka za kanisa.

Pia, ripoti ya uchunguzi ya TRA ilibainisha kuwa Askofu Kakobe mbali na kupeleka fedha benki kuna fedha huwa zinahifadhiwa kwenye majaba na ndoo na kwamba, kanisa hilo lilikwepa kulipa kodi Sh20.8 milioni katika shughuli zake za kiuchumi, lakini zililipwa baada ya uchunguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com