Kama walivyozaliwa wawili kwa pamoja, ndivyo walivyofariki dunia.
Ni watoto pacha wenye umri kati ya miaka minne na mitano, Nyakato (mvulana) na Nyangoma (msichana) wa Kijiji cha Butahyaibeba wilayani Bukoba waliouawa kwa kuchinjwa na mtu anayedhaniwa kuwa baba yao mzazi usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa Dickson Barongo, mwenyekiti wa kitongoji cha Bulambizi ambako mauaji hayo yametokea, watoto hao walichinjwa na kutenganishwa vichwa na viwiliwili.
“Nilikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio baada ya kufuatwa nyumbani na mtoto aliyenusurika,” alisema Barongo.
Hata hivyo, alisema mama wa watoto hao alikimbia wakati mume wake akifanya tukio hilo ili kujinusuru.
Barongo alisema kabla ya kufanya mauaji hayo, mzazi huyo aliwachukua watoto hao na kuwafungia chumbani.
“Chanzo cha mauaji hayo kinahusishwa na ugomvi kati ya wanandoa hao,” alisema.
Inadaiwa kuwa baada ya wanandoa hao kutengana, mwanamke alienda kuishi kwao akiwaacha watoto na baba yao.
“Lakini juzi alifika hapo kwa mume wake akawaomba wakamtembelee Alhamisi ya wiki iliyopita na jana (Jumamosi) alikuwa amewarudisha kwa baba yao,” alisema.
“Mume alimruhusu mzazi mwenzake kuondoka na watoto hao na siku ya tukio alikuwa amewarejesha kwa baba yao lakini baba alimzuia mke wake kuondoka na akafunga mlango, lakini wakati wa vurugu hizo alifanikiwa kutoroka,” alisema.
Barongo aliongeza kuwa walimpata mtuhumiwa kwa njia ya simu na akawajibu kuwa bado hajamaliza kazi na baadaye simu yake haikupatikana.
Msimamizi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Gloria Mpango alisema uchunguzi wa awali unaonyesha watoto hao walichinjwa na kutenganishwa vichwa na viwiliwili na wanasubiri taratibu za polisi kabla ya ndugu kuruhusiwa kuchukua miili kwa mazishi.
Na Phinias Bashaya, Mwananchi
Social Plugin