Wanaume zaidi ya kumi wameibuka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulalamika kupokwa watoto, huku mamia ya wanawake wanaodai kutelekezewa watoto wakiendelea kumiminika kwenye ofisi za mkuu huyo wa mkoa.
Wanaume hao ambao wamefika leo Jumanne Machi 10, 2018 wamesema hawashindwi kulea watoto isipokuwa wake zao wamewapoka kwa madai ya umasikini.
Wamesema kama Makonda ameamua kuwasaidia wanawake basi ajue wapo wanaume wanaolia kunyanyaswa na wake zao.
"Mke wangu alinikimbia nilipougua miguu kiasi cha kushindwa kutembea, aliondoka na watoto wangu wote watatu, nimekuwa mtu wa mawazo kiasi cha kupata vidonda vya tumbo naomba awarudishe," amesema Tito Chemba, mkazi wa Kijichi jijini Dar es Salaam.
Tito (35), amesema ujio wake kwa Makonda ni kutaka kurejeshewa wanawe wanaoishi Bukoba kwa ndugu wa mkewe.
Mwanamume mwingine, Edmond Mbisho amesema mkewe aliondoka na mtoto wake tangu akiwa na miaka mitatu na sasa ana miaka sita.
“Ninachoomba ni kupata mwanangu si kingine, kwa sasa mwanamke anaishi na mtu mwingine," amesema.
Mwanamume mwingine, Vedasto Mdesa mkazi wa Iringa amesema watoto wake watatu waliozaliwa kwa pamoja walichukuliwa na ndugu wa mkewe na kupelekwa Urusi.
"Nilipokwa watoto kisa mimi ni masikini, hivi sasa naishi kwa tabu na sababu kubwa ni umasikini na wanasema sijasoma. Huyo mwanamke ana shahada na mimi ni mpiga picha nisiye na elimu," amesema.
Mkazi wa Kitunda, Mohammed Juma naye ametinga katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akidai kunyanyaswa na mke wake.
Juma amesema amefukuzwa na mke wake katika nyumba ya urithi, kisha mwanamke huyo kuwafukuza wazazi wake na watoto wa Juma.
“Wanaume tuna matatizo mengi lakini hatuyasemi, hatuyazungumzi bayana, imefikia wakati tupate nafasi tutoe manung’uniko yetu,” amesema.
Amesema wanawake wana umoja ndiyo maana wanaweza kusema matatizo yao, lakini wanaume nao wanafanyiwa mambo ya ajabu lakini wanavumilia kwa kuwa hawana pa kusemea.
“Nimejenga nyumba kwa fedha zangu, kwa sababu nafanya kazi kwa Wahindi, lakini mwanamke amenidhulumu na akafikia hatua ya kuwafukuza wazazi wangu na watoto wake wa kufikia,” amesema.
Wake kwa waume wamefurika katika ofisi ya Makonda leo baada ya mkuu huyo wa mkoa kuagiza wenza waliotelekezwa na kuachiwa watoto, wafike ili wapewe msaada wa kisheria.
Chanzo- Mwananchi