Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NDAGALA AKABIDHI MABATI,MIFUKO YA SARUJI KUNUSURU WANAFUNZI 346 KAKONKO

Jumla ya wanafunzi 346 wilayani Kakonko mkoani Kigoma wa kidato cha kwanza waliokuwa hawajajiunga na kidato cha kwanza kutokana na shule walizopangiwa kuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa wanatarajia kujiunga na kidato hicho mwishoni mwa Mwezi Aprili mwaka huu kutokana na jitihada za wananchi na mchango wa serikali wilayani humo.

Akitoa takwimu hizo baada ya kupokea msaada wa mifuko 100 ya saruji na mabati 60 yaliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo Kanali Hosea Ndagala kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba vya madarasa vitano, Afisa elimu sekondari wilayani humo, Christopher Bukombe alisema kati ya  wanafunzi 1714 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza walioshindwa kuripoti ni 346 waliopangiwa katika shule ya Kanyonza, Muhange na Gwanumpu ambapo baada ya Mwezi huu kuisha Wanafunzi watajiunga kutokana na changamoto kutatuliwa.

Alisema katika shule ya Kanyonza kuna wanafunzi 78, Muhange 97 na Gwanumpu 171 ambapo kutokana na upungufu huo walianza kuhamasisha wananchi kuchangia na serikali imetoa shilingi milioni nane katika shule mbili za Kanyonza na Gwanumpu na shilingi milioni nne kwa shule ya Muhange.


Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alikabidhi mabati 60 na mifuko 100 ya saruji katika kuhakikisha anaunga mkono jitihada za wananchi walizoonyesha na kuwapongeza watendaji wa kijiji, madiwani pamoja na wenyeviti wa vijiji kwa juhudi kubwa walizozionyesha za kuwashawishi wananchi kujitoa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi waanze kupata elimu kama wengine.

Mkuu huyo alisema serikali inatamani kuona kila mtoto anapata elimu, na ni jukumu la Wazazi wajitoe kutatua baadhi ya changamoto zinazo jitokeza kwa kuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu pamoja na kutatua changamoto zingine na kuwaagiza wananchi wengine kuiga mfano wa wananchi hao kwa kuwa serikali inapenda wananchi wajitolee katika kuchangia na kushirikii kwenye shughuli za maendeleo.

"Niwaombe wananchi mnapoambiwa elimu bila malipo sio kwamba hata kujitolea kwenye ujenzi mshindwe,  watoto ni wa kwenu lazima mnapoona serikali haijakamilisha jambo flani mfanye wenyewe ,suala hili ni letu sote lazima wanafunzi wote wapate elimu ni haki yao hakuna urithi mwingine tutakaowaachia watoto wetu zaidi ya elimu lazima mtambue kuna michango mingine wananchi wanatakiwa kuchangia kuhakikisha changamoto hizi zinakwisha", alisema Kanali Ndagala.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Gwanumpu, Toy Butono kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Kakonko alimshukuru mkuu wa wilaya hiyo na kuwaomba wananchi kuendelea kuchangia huduma za maendeleo kwakuwa jukumu la ujenzi wa taifa ni la wananchi wote lazima wajotoe kwaajili ya maendeleo.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikabidhi mabati na mifuko ya saruji - Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com