Mtoto wa miezi miwili jina limehifadhiwa mkazi wa Kitongoji cha Unyanyembe kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga amenusurika kufa baada ya kunyeshwa sumu ya panya na baba yake mzazi Edson Timotheo Damiani (37) kwa kile kilichoelezwa ni kutaka kuficha siri ili mkewe asijue kama amezaa mtoto mwingine nje ya ndoa.
Akielezea tukio leo Aprili 12,2018 Mama mzazi wa mtoto huyo Maria Shija amesema lilitokea Mach 24 mwaka huu majira ya saa tatu usiku ambapo baba wa mtoto huyo alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo kwa ajili ya kumsalimia mtoto wake ndipo akamnywesha sumu ya panya kwa lengo la kumuua.
Amesema wakati kitendo hicho kikifanywa na mzazi mwenzake huyo alikuwa akimtuma maji ya kunywa mara kwa mara ambapo siyo kawaida yake na aliporudisha kikombe ndani ndipo akasikia harufu ya dawa ya panya na aliporudi kwa mtoto haraka akamkuta ameanza kutoa mapovu na mwanaume kukimbia na kopo la sumu ya panya.
“Nilipobaini kuwa mtoto kapewa sumu nikakimbia kwa jirani anayefuga ng’ombe, ndipo nikachukua maziwa nikamnywesha, na baadae nikachukua bodaboda hadi kituo cha polisi kupewa RB na kisha kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kupatiwa matibabu, na sasa mtoto wangu ni mzima”,amesema Shija.
"Mwanaume huyu ni katibu wa CCM kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga na wakati ananitongoza aliniambia hana mke na baada ya kuzaa huyu mtoto ndipo akasema ana mke na hamtaki kwani atavunja ndoa yake, na ndiyo chanzo cha kutaka kumuua kwa kumywesha sumu ya panya”,aliongeza.
Naye mtu wa karibu na familia hiyo Jumanne Kagusa, amesema baada ya kuona mtuhumiwa huyo anazagaa mitaani na kutochukuliwa hatua yoyote ya kisheria ndipo naye akafika kufuatilia suala hilo kwa jeshi la polisi na hatimaye juzi akakamatwa na kuswekwa rumannde.
Kwa upande wake kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa anashikliwa na kubainisha kuwa upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Imeandikwa na Marco Maduhu- Malunde1 blog & Shinyanga News blog
Social Plugin