Watu zaidi ya 41 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha ndani ya kipindi cha takriban miezi miwili nchini Rwanda.
Wizara inayohusika na kupambana na majanga imetoa wito ikiwataka wananchi wanaoendelea kuishi katika maeneo hatarishi kuhama.
Ripoti kuhusu maafa yanayotokana na mafuriko ya mvua zimekuwa zikitolewa katika miaka ya hivi karibuni na mara nyingi Serikali imekuwa ikiahidi kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo. Hata hivyo, mpaka sasa hatua hizo hazijaweza kulipatia tatizo hilo suluhu ya kudumu.
Wananchi wamedai kuwa janga la mafuriko linalosababisha maafa na hasara, kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangiwa na ukosefu wa sera bora ya mipango miji hali inayosababisha kila mvua ikinyesha maji kuwasomba watu na mali zao.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (Voa), ameripoti kuwa mashamba mengi yamefunikwa na udongo na mazao kama vile miwa, nyanya, viazi yametoweka.
Pia, kumearifiwa kuwepo kwa uharibifu mwingine wa miundombinu huku nyumba kadhaa za raia zikianguka.
Kutokana na maafa hayo wananchi wameomba msaada wa chakula kutoka serikalini.
Baadhi ya wananchi wanataka mifereji iliyoelekezwa katika maeneo yao, ielekezwe maeneo mengine kwa kuwa ndiyo inayosababisha matatizo hayo.
Lakini wizara inayopambana na majanga inasema licha ya kutoa misaada, bado wananchi wana jukumu la kuchukua tahadhari na kinga.
Serikali imesema licha ya vifo hivyo, watu 162 walijeruhiwa na mvua hizo huku makazi 3,000 yakisombwa na maji sambamba na ekai 1,751 zilizoharibiwa na mvua.
Mwezi uliopita watu 16 walifariki dunia kwa mpigo baada ya kupigwa na radi walipokuwa kanisani magharibi mwa nchi hiyo.
Social Plugin