Mamia ya wanawake waliotelekezwa baada ya kuzalishwa na waume zao wamejazana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyetangaza kuanza kuwasikiliza.
Kumekuwa na mafuriko ya wanawake wanaoingia kwa kusukumana kwenye ofisi hizo hali iliyowalazimu walinzi kufunga geti ili walio ndani wahudumiwe.
Wanasheria na wafanyakazi wengine wa ofisi hiyo wanaendelea kuwasikiliza wanawake hao wengi wao wakiwa wamebeba watoto wao.
Wakizungumza leo, Aprili 9 wanawake hao wamesema wingi wao unaweza kusababisha baadhi yao kushindwa kusikilizwa.
"Nilitelekezwa na watoto wanne kwenye nyumba ya kupanga, nimekuwa kama ombaomba nashukuru Makonda ameona kilio chetu lakini kwa umati huu naogopa sana,"amesema mwanamke mmoja.
Wapo waliolala kwenye ofisi hizo huku wengine wakianza kuwasili tangu saa tisa za usiku.
Vimetengwa vyumba maalum zikiwamo kumbi zilizo katika ofisi hizo kwa ajili ya kusikiliza kilichowasibu wanawake hao.
Na Tumaini Msowoya, Mwananchi
Social Plugin