Mbunge wa Kilwa Kusini kupitia chama cha CUF Suleiman Bingara maarufu kwq Jina BWEGE amesema anashindwa kuelewa kauli ya Waziri Mkuu kuwa nchi ipo salama, kutokana na vitendo vinavyoendelea kujitokeza.
Akizungumza leo Bungeni Suleiman Bungara amesema matukio ya mauaji na unyanyasaji yanayofanywa na watu wanaoaminika ni polisi, yanafanya nchi kuwa sio sehemu salama hivyo hakubaliani na kauli hiyo, huku akitolea mfano wa tukio lililofanywa na polisi huko Chumo wilayani Kilwa.
“Askari walikwenda Chumo msikitini, wakapiga risasi wakachukua watu 10 tumefika damu zimetapakaa, walivyorudi mmoja kafa, mmoja hana jicho, mmoja wakamnyoa ndevu kwa kumchoma moto, mnapotuambia nchi hii ina amani na utulivu mimi siwaelewi, nchi imeharibika, tumetengenezewa waislamu wakisema jambo kuhusu waislamu wenzao tunaambiwa sisi magaidi, ndio maana mashehe hawasemi, akipigwa muislam akisema tunaambiwa magaidi”, amesema Bungara.
Bungara ameendelea kwa kusema kuwa ili nchi iwe yenye utulivu na kuishi kindugu, lazima misingi ya kidemkrasia ifuatwe, na ndipo tutakapoweza kutekeleza mengine.
“Nchi yetu kama haitakuwa na uhuru na haki, basi undugu na amani hautakuwepo, kwa mujibu wa katiba yetu”, amesema Mbunge huyo maarufu kwa jina la Bwege.
Social Plugin