Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LORI LA MAFUTA LAUA MKURUGENZI HALMASHAURI YA KONGWA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa mkoani Dodoma, Mhandisi Ngusa Izengo anadaiwa kufariki dunia baada ya gari lake kuangukiwa na lori la mafuta usiku wa kuamkia leo Aprili 15, 2018 katika eneo la Chalinze Nyama nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Taarifa ya masikitiko ya serikali imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo wakati akizungumzia kifo hicho. 

Taarifa ya ajali hiyo zinasema kwamba gari la Mkurugenzi huyo, lililaliwa na lori la mafuta katika eneo la Chalinze Nyama, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

 Taarifa zaidi zinasema kwamba gari dogo alilopanda mkurugenzi huyo, lenye namba za usajili T619 DMA aina ya Toyota Crown Athlete, liliangukiwa na lori lililobeba mafuta eneo la Mbande Makaravati.

Ajali hiyo imethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Muroto na kuahidi kutoa taarifa kamili baadaye. 

“Nitatoa taarifa kamili shughuli ya uokaji itakapomalizika maana mpaka muda huu tumetoka eneo la tukio tumeshindwa kujua kuna watu wangapi ndani ya gari hilo lililoangukiwa. “Tunakwenda TEMESA kutafuta ‘grinder machine’ ili tuweze kujua idadi kamili ya miili iliyopo ndani ya gari,” alisema Muroto.

 Hata hivyo, baadaye wasaidizi wa kamanda huyo walisema kwamba shughuli ya kutafuta chanzo cha ajali, kilikuwa kinaendelea na kwamba wapo hospitali kwa ajili ya majeruhi.

Inaaminika dereva wa lori, amejeruhiwa na amekimbizwa hospitalini. Taarifa hiyo ya kifo imewasikitisha wakurugenzi wenzake waliomo Mkoa wa Dodoma, ambao walisifu uchapaji kazi wake na kusema mkoa umeondokewa na mmoja wa watu wanaowajibika katika nafasi zao.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba alisema Izengo alikuwa mchapakazi, mwenye busara, upendo kwa watu na mcheshi na hakuwa na makuu na jamii itamkosa sana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bahi, Rachel Chuwa alisema Ngusa alikuwa kijana mchapa kazi, mpenda watu, mtu mpole, mwelewa wa mambo mengi, mcheshi, asiye na majivuno na kusema watamkosa katika utendaji.

 “Juzi tu Ijumaa tulikuwa naye katika Kikao cha Kamati ya Sherehe Taifa kilichofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kupanga mikakati ya kufanikisha Sherehe za Muungano wa Tanzania na Zanzibar inayotarajiwa kufanyika 26/04/2018 Dodoma. Alikuwa mzima wa afya, mwenye kujiamini katika mipango yake ya kuiendeleza Kongwa, “ alisema Chuwa.

Alisema alikuwa amezoeana na mkurugenzi huyo na walikuwa wakipigiana simu ili kushaurina namna bora ya kutekeleza maagizo mbalimbali ya serikali na wananchi. “ Kifo chake kimenisikitisha sana. Alikuwa bado anahitajika na familia yake, wana Kongwa, wana Dodoma na Taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu amrehemu, amsamehe dhambi zake zote na kuilaza mahali pema peponi Roho yake. Tulishirikiana naye, sisi tulimpenda, Mwenyezi Mungu amempenda zaidi.

Kalale pema peponi Ngusa, tutakukumbuka kwa mema mengi. Wana Kongwa na Dodoma kwa ujumla tumepotelewa na mtu mwema sana,” alisema Chuwa. Ngusa alichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kongwa na Rais John Magufuli Julai 7, 2016 wakati wa uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji 5, Manispaa 21, Miji 22 na wilaya (DC) 137 za Tanzania Bara. Aliapishwa Ikulu Dar es Salaam Julai 12, 2016. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa msaidizi wa waziri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com