"MSHIKAKI" WAUA WANAWAKE WAWILI KAHAMA


Wanawake wawili wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wameipanda kwa mtindo wa “Mshikaki” kuanguka kutokana na mwendokasi wa mwendeshaji katika eneo la Zongomela Mbugani kata ya Zongomela wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga. 

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule ajali hiyo imetokea jana Aprili 3,2018 saa moja na dakika 45 usiku katika barabara ya kuelekea Nyandekwa pikipiki ikitoka kijiji cha Igunda kuelekea Kahama Mjini. 

Amesema pikipiki hiyo yenye namba za usajili T.185 CJF aina ya Sanlg mali ya mtu asiyefahamika,ikiendeshwa na dereva asiyefahamika ilianguka na kusababisha vifo vya wanawake wawili. 

Amewataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Mwanaisha Kabichi Maganga (32) mkazi wa Nyasubi na Zawadi Stanley (28) mkazi wa Nyihogo ambao walikuwa wamebebwa kwenye pikipiki hiyo. 

“Chanzo cha ajali ni mwendokasi wa mwendesha pikipiki ambaye pia yeye na abiria wake hawakuzingatia sheria,taratibu,kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa kila mara kupiga vita na kukataza upakiaji/upandaji wa abiria wawili kwenye pikipiki moja ya magurudumu mawili maarufu kama “Kupakia mishikaki”,amesema Kamanda Haule. 

Ameongeza kuwa juhudi za kumtafuta mwendesha pikipiki aliyekimbia baada ya ajali na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mji wa Kahama. 

Na Kadama Malunde – Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post