Zaidi ya nyumba 120 zimeharibika vibaya katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa muda wa siku mbili mfululizo.
Kaimu Mkurugenzi Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu, Aprili 16 amesema kuwa takwimu hiyo ni ya awali tu ila wanatarajia huenda ikaongezeka zaidi kutokana na maeneo mengi bado hayajafanyiwa uhakiki.
Amesema miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika na mvua hizo ni pamoja na Amani Kwawazee, Daraja Bovu, Seblen, Mwanakwerekwe, Fuoni pamoja na Kibonde Mzungu.
Amesema mbali ya maeneo hayo lakini pia kuna baadhi ya miundombinu ya barabara nayo imeharibika ikiwamo barabara ya Fuoni pamoja na Mwanakwerekwe ambayo imefungwa kabisa kutokana na kujaa maji maeneo yote na kusindikana vyombo vya moto pamoja na wananchi kushindwa kupita.
Amesema hivi sasa wanaendelea kukusanya taarifa kutoka kila pande ya miji ya Zanzibar ili kujua athari kwa ujumla pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na maafa Zanzibar.
Na Haji Mtumwa, Mwananchi