Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Kheri James amesema kwamba kitendo cha watu kulalamika kuhusu serikali kununua ndege wakati bado kuna hali duni, si sahihi kwani kazi ya serikali sio kugawa riziki.
Kheri James ameyasema hayo alipokuwa katika kipindi cha Kikaangoni cha EA Television, na kusema kwamba kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira ili wananchi waweze kupata riziki yao kwa kazi wanazofanya, na sio kuwagawia pesa kila mmoja kwa lengo la kupunguza umasikini.
Kheri ameendelea kwa kusema kwamba hali duni ya maisha ya baadhi ya watu ni jambo la kawaida kwani Mungu ndiye amepanga, na sio Rais, lakini kuna watu wanataka Rais afanye kazi ya Mungu ya kugawa riziki.
“Unajua kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira kwa kila mtu kupata mkate wake wa halali, sio kazi ya serikali kugawa riziki.
"Sisi kama chama kazi yetu ni kutengeneza mazingira kwamba kila raia kazi yake anayoifanya inaweza kumuingizia kipato.
"Hatuwezi kama serikali tukaenda kumpelekea hela mtu mmoja mmoja, hatuwezi kufanya kazi ya Mungu, kuna watu wanataka Rais awe anafanya kazi ya Mungu.
"Kuna watu ni wa mchicha, na kuna watu ni wa kuku, Mungu kashapanga, na mimi niseme kwa mazingira tuliyonayo tupigane na serikali itengeneze mazingira ya watu kupata riziki”, amesema Kheri James