Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu wanne kwa tuhuma ya kukamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kwenye viroba vitano ikiwa na uzito wa kilo 98 kutoka kata ya Kagongwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwenda Jijini Dar es salaam.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Aprili 16, 2018,Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa polisi Simon Haule alisema watu hao walikamatwa Aprili 15,2018 majira ya saa 12 asubuhi katika geti la maliasili barabara ya Kahama - Tinde kata ya Itogwanholo wilaya ya Kipolisi Msalala.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Simon Juma Kashindye (46) mkazi wa Nyanshimbi Shinyanga vijijini, Lameck Nicombolwe (44) Kulwa Nelson (21), na Shabani Nurdin(20), wote hao watatu wakiwa wakazi wa Jijini Dar es salaam.
Alisema watu hao walikamatwa wakisafirisha bangi hiyo kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 872 CVS Coaster mali ya Precabi mkazi wa Dar es salaam.
“Bangi hii kama mnavyoiona imefungwa kwenye viroba 5 na ina uzito wa kilo 98 na watuhumiwa hawa walikuwa wakisafirisha kwenda Jijini Dar es salaam kwa kutumia gari hiyo ya abiria, na tunaendelea kuwashikilia kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikalimika watafikishwa mahakamani kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Haule.
“Na uchunguzi ukikamilika na watu hawa watafikishwa mahakamani kuchukuliwa hatua kali za kisheria, na mahakama ndiyo itatoa amri ya bangi hii kuharibiwa, nasi ndipo tutakapoiteketeza kwa moto,” aliongeza.
Naye mmoja wa watuhumiwa hao Lameck Nicombolwe ambaye ni dereva wa gari hilo alisema wao walikodiwa kuleta msiba katika Kata hiyo ya Kagongwa, ndipo wakapata tenda ya kupakia bangi hiyo na kuambiwa kuwa ni tumbaku, lakini walishangaa mhusika wa mzigo huo ghafla anashuka kwenye gari na kutokomea huku wao wakikamatwa.
Aidha kufuatia tukio hilo Kamanda alitoa wito kwa wananchi mkoani Shinyanga kuachana na tabia ya kujihusisha na biashara haramu pamoja na kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa za wahalifu ili wapate kushughulikiwa mapema na mkoa ubaki kuwa salama.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule akielezea namna walivyokamata dawa za kulevya aina ya Bangi.
Askari polisi wakiangalia bangi hiyo
Askari polisi wakifungua viroba vitano walivyo vikamata vikiwa na bangi.
Bangi ikiwa kwenye kiroba.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule akihoji watuhumiwa waliokamatwa na bangi.
Lameck Nicombolwe ambaye ni dereva wa gari hilo akijitetea
Watuhumiwa waliokamatwa na madawa hayo ya kulevya aina ya bangi wakijieleza.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule, akionyesha gari aina ya Toyota Coaster yenye namba za usajili T. 872 CVS Mali ya Precabi mkazi wa Jijini Dare es salaam ambayo imetumika kusafirisha bangi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule akitoa taarifa hiyo ya kukamata bangi kwa vyombo vya habari.
Baadhi ya waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari mkoani Shinyanga wakiwa katika wakichukua matukio
Baadhi ya waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari mkoani Shinyanga wakiwa wakiandika dondoo.
Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga News Blog