Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambaye alikuwa lindo, jana alfajiri aliwashambulia mwenzake, raia na kutishia kumfyatulia risasi mkuu wake nje ya benki ya CRDB jijini Tanga na jitihada za kumdhibiti zikasababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi limeahidi kutolea ufafanuzi tukio hilo mara baada ya kukamilisha uchunguzi wake.
Wakisimulia jinsi tukio hilo lilivyokuwa, wananchi wanaoendesha shughuli zao jirani na benki hiyo iliyo Tarafa ya Ngamiani, walisema mashambulizi ya risasi yalianza saa 11.30 alfajiri baada ya kusikika kelele ya msichana eneo la kuegeshea magari ya benki hiyo.
Walisema kelele hizo zilisababisha mmoja wa askari aliyekuwa zamu kuzunguka kushuhudia nini kinaendelea, ndipo akamkuta askari mwenzake aliyekuwa naye zamu akiwa na msichana, huku msichana huyo akipiga kelele.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, askari aliyefahamika kwa jina la Valerian Temba alimyang’anya mwenzake silaha aliyokuwa ameshika na kisha kumfyatulia risasi iliyomjeruhi mguuni.
“Mara askari waliokuwa wakilinda benki ya NMB ya jirani wakakimbilia eneo la tukio, lakini nao wakatishiwa kupigwa. Ndipo wakampigia simu mkubwa wao wa FFU ambaye alikuja haraka na kukuta tafrani hiyo, ”alisema mtu aliyejitambulisha kwa jina la Charles Mathias.
Shuhuda huyo alisema wakati tafrani hiyo ikiendelea, askari walizungushia kamba eneo lote la benki ya CRDB kama ishara ya kuzuia watu wasipite kwa kuwa Temba alikuwa ameelekeza bunduki akitishia kuua yeyote ambaye angemsogelea.
Mashuhuda hao walisema, mkuu wao FFU aliwasili na kumsihi askari huyo kusalimisha silaha lakini hakufanikiwa.
“Yule askari alisisitiza kuwa angemuua hata yeye (mkuu wake) endapo angemfuata,” alisema
Mashuhuda hao wameeleza kuwa askari huyo alianza kurusha risasi hovyo zilizoharibu magari na baadhi ya nyumba za jirani, ndipo askari wenzake walipoamua kumdhibiti ili asisababisha madhara zaidi.
Inadaiwa kuwa askari wenzake walifyatua risasi na moja ikamjeruhi na alifariki baadaye wakati akipata matibabu.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema waliposikia milio ya risasi walidhani ni sehemu ya mazoezi ya polisi ambao Jumamosi walikuwa wakiadhimisha Siku ya Familia.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema atatolea maelezo ya tukio hilo mara baada ya jeshi la polisi kukamilisha uchunguzi kwa mujibu wa taratibu za kijeshi.
“Watu wanaeleza wanavyoona, lakini niseme tu kwamba fanyeni subira hadi tutakapokamilisha uchunguzi kama ambavyo taratibu za kijeshi zilivyo. Nitawaeleza kila kitu hakuna kitakachofichwa,” alisema Bukombe.
Na Burhani Yakub, Mwananchi
Social Plugin