Raia wa kigeni wanaoshi mkoani Kigoma wametakiwa kuacha kuingiliza zoezi la uandikishwaji wa vitambulisho vya taifa linaloendelea mkoani mumo, kwa kuwa zoezi hilo ni haki kwa watanzania pekee.
Rai hiyo ilitolewa jana wilayani Kasulu na Mmoja wa wakimbiza Mwenge wa uhuru Dominik Njunwa wakati akitoa ujumbe wa Mwenge, katika kijiji cha Shunga wakati wa ufunguzi wa Bwalo la kulia chakula katika Shule ya Sekondari Muyovozi ambapo aliwaomba Watanzania waishio jirani na nchi ya Burundi kuwafichua wale wote wasio raia wa Tanzania watakaojitokeza kujiandikisha katika zoezi la upatikanaji wa vitambulisho vya taifa.
Njunwa alisema hairuhusiwi raia yeyote asie Mtanzania kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya taifa, kwa kuwa vitambulisho hivyo vinatolewa kwa Watanzania pekee na ni kosa kubwakwa raia wa nchi nyingine kupata kitambulisho hicho.
Aidha Kaimu mkuu wa wilaya ya Kasulu ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala aliwataka viongozi wa vijiji na mitaa kuacha kuhujumu zoezi hilo kwa kuwaingiza watu wasio Watanzania ili waweze kupata vitambulisho na kwa atakae bainika anafanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Pia mkuu huyo aliwataka wananchi kuwafichua wale wote wanaowahofia kuwa sio raia wanaojitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya taifa na kuwaripoti kwa vyombo husika ili kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria na waondolewe katika zoezi hilo.
Kanali Ndagala alisema zoezi hilo ni kwa watanzania tu wanapopatiwa raia wasio wa Tanzania ni kosa na inaweza kuleta shida katika taifa la Tanzania na kuwaonya kuwa makini ili kuendeleza hali ya usalama hasa kwa mikoa iliyopo karibu na nchi jirani za Burundi na Congo.
"Kuanzia Mwakani Mtanzania akiwa na kitambulisho cha Taifa anauwezo wa Kupata hati ya kusafiria wanapopata watu wasio Raia wakipata hati zetu za kusafiria inatupa shida sana na wanatumia kwa kufanya uhalifu jambo ambalo sio zuri katika taifa letu marufuku kabisa kwa raia asie Mtanzania kuchukua kitambulisho", alisema Ndagala.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake mkoani Kigoma wilayani Kasulu umekagua na kuzindua miradi 13 yenye thamani ya zaidi ya bilioni tano miradi hiyo ni ya maji, afya na maji na sambamba na miradi hiyo Mwenge huo umezindua kituo cha afya katika kijiji cha Shunga kilichojengwa na Kanisa la Anglikana.
Social Plugin