RAIS MAGUFULI ATAKA BEI YA UMEME KUSHUKA

Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuanza kufikiria uwezekano wa kushusha bei ya umeme.


Pia, ameitaka wizara hiyo na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuondoa changamoto za kuwaunganishia umeme wananchi na hasa zinazohusu rushwa.


Rais Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozindua kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 240.


Alisema kupatikana kwa umeme wa kutosha ndiko kutakakofanikisha Tanzania ya viwanda.


Dk Magufuli alisema kwa sasa mahitaji ya nchi ni Megawati takriban 1,40O lakini uzalishaji umefikia Megawati 1,515.3.


“Bado tunahitaji umeme wa kutosha tuongeze uzalishaji,” alisema.


Alisema baada ya gharama za kuunganisha umeme kushushwa, “Wizara ya Nishati muanze kufikiria sasa hata kushusha bei ya umeme, haiwezekani tukawa na umeme mwingi halafu bei ikaendelea kubaki juu.”


Rais alisema licha ya gharama ya kuunganisha umeme kupungua, kumekuwa na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wananchi kuombwa rushwa.


“Wizara ya Nishati na Rea, hakikisheni mnaongeza kasi ya kuunganisha umeme na shughulikieni malalamiko ya wafanyakazi kuomba rushwa, yashughulikieni hayo,” alisema Rais Magufuli.


Bei ya sasa ya umeme ilitangazwa Aprili Mosi, 2016 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ambayo licha ya kushuka, huduma ya malipo (service charge) ya Sh5,520 na Sh5,000 iliondolewa.




Taasisi kulalamikiana


Akijibu ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka la Serikali kulipunguzia tozo shirika lake, Rais Magufuli alisema kumekuwa na malalamiko kati ya taasisi moja na nyingine serikalini.


Alisema taasisi au mamlaka za Serikali zinatakiwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na hasa inapotekelezwa miradi mikubwa ya Taifa. “Mawaziri, wakurugenzi, wenyeviti wa bodi msiache kuwasiliana ninyi kwa ninyi, kama unaona unakwamishwa na taasisi nyingine, mambo kama haya nikisikia huwa yananiudhi, lugha ya mitaani yananiboa kwelikweli.


“Shirikianeni kwani mnapokwamishana mnawacheleweshea wananchi maendeleo,” alisema akitoa mfano kuwa hivi karibuni alipokwenda Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuzindua magari 181 ya kusambaza dawa, waliilalamikia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kukwamisha mizigo bandarini


Dk Mwinuka aliiomba Serikali kuipunguzia Tanesco tozo za uingizaji vifaa vya kuboresha miundombinu ya umeme ili kupunguza gharama za miradi. Alisema gharama za tozo zinakwamisha umalizaji miradi kwa wakati kutokana na kutokuwa na fedha.


Alisema pamoja na mradi kufadhiliwa na Serikali na msaada wa mkopo nafuu wa Japan, Tanesco inalazimika kulipa gharama kubwa ikiwamo ya malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo imefikia Sh136 bilioni.


Alisema tozo ya kupitisha mizigo mikubwa katika barabara za Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) imefikia Sh5.6 bilioni, tozo ya reli Sh186 milioni na gharama za kutoa mizigo bandarini Sh12.23 bilioni.


Alisema shirika linashindwa kulipa fedha kwa wakati hivyo mizigo kukaa muda mrefu bandarini na gharama kuongezeka.


“Tunaiomba Serikali iangalie namna ya kuondoa tozo hizo ili kutusaidia kukamilisha miradi kwa wakati,” alisema Dk Mwinuka.


Kuhusu mradi huo wa Kinyerezi II, Dk Mwinuka alisema umegharimu dola 344 milioni za Marekani sawa na Sh758 bilioni.


Kati ya fedha hizo, alisema Tanzania imetoa Sh154 bilioni na zilizobaki ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Japan.


Awali, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi kadhaa ya umeme lengo likiwa ifikapo mwaka 2020 uzalishaji ufikie Megawati 5,000 na mwaka 2025 zifikie 10,000.


Alisema katika miradi ya kuzalisha umeme, Kinyerezi III itazalisha umeme Megawati 600 na Kinyerezi IV itazalisha Megawati 350 na ikikamilika kutakuwa na jumla ya Megawati 1,992.


Waziri Kalemani alisema uzalishaji wa umeme wa maporomoko ya Rufiji wa Megawati 2,100 ukikamilika utaongeza nishati hiyo katika gridi ya Taifa, “Tukikamilisha tutaanza mchakato wa kuusafirisha ili ukatumike katika reli ya kisasa ya SGR,” alisema.


Kuhusu kuunganishwa kwa umeme, Waziri Kalemani alisema kwa miaka miwili, wameunganishiwa wateja 250,000.


Alisema kwa mwaka huu, vijiji 82 vimeunganishiwa wakiwamo wakazi wenye nyumba za udongo.


“Tunafanya hivi kwa kuwa Rais umetuagiza kuwaunganishia wananchi wote kwani nyumba ni nyumba,” alisema.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post