Rais John Magufuli jana alishangaa maaskofu nchini kutoa waraka sasa na akasema hapendi kuuzungumzia bali ataendelea kuisimamamia nchi aliyokabidhiwa na wananchi.
Rais Magufuli alishangaa ni kwanini maaskofu hao hawakutoa waraka wakati wa mauaji ya kinyama ya watu wasio na hatia ya Kibiti mkoani Pwani, na kuhoji kama marehemu hao walistahili kuuawa.
Kati ya mwaka 2015-2017, kulikuwa na matukio ya mauaji mfululizo ya watu zaidi ya 40, wengi wakiwa viongozi na askari polisi mkoani Pwani lakini sasa yamekomeshwa kwa jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza jana wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa usimikaji wa mfumo wa rada nne za kuongozea ndege jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema uchumi unakuwa vizuri kutokana na kubana njia zote za wizi wa mali ya umma uliofanywa na wachache.
"Ninafahamu hata makanisani zaka zimepungua maana zilikuwa zinatolewa na mafisadi... Watanzania tusimame twende mbele kwa ajili ya maendeleo yetu," alisisitiza Rais Magufuli na kueleza zaidi:
"Hakuna waraka uliotoka kwa watu wa Kibiti waliouawa, kwahiyo wao ni sawa kuuawa?
"(Hata hivyo) Sipendi kulizungumzia maana halina msingi... serikali ipo nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote.
"Wengine nawaangalia, nawachekiii nasema iii," alisema Rais Magufuli na kusababisha mamia ya watu waliohudhuria uzinduzi huo kuangua kicheko.
Aidha, Rais Magufuli alisema kwa miaka mingi nchi imekuwa ikitegemea wafadhili lakini kwa sasa inakwenda vizuri.
"Watanzania waendelee kuliombea taifa na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, napenda mjue kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakwenda mbele," alisema Rais Magufuli.
"Nawaambiwa Watanzania tunaenda pazuri, kazi ya uongozi ni zuri sana... usiposimama na kumtegemea Mungu unaweza kukata tamaa.
"Nawaambia seriali ipo, haijalala na haitalala, usione simba amelala ukawa unagusagusa mkia wake. Watanzania tembeeni kifua mbele, tupo pazuri sana, mtapigwa vita na watu wa nje.
"Tusimame imara, tusonge mbele na tumtangulize Mungu ambaye ni wa kweli kwa watu wa kweli na tutafanikiwa."
Alisema nchi inakwenda vizuri na kutaka Watanzania kutembea kifua mbele kwa kuwa uwezo wa nchi ni mkubwa na wa maajabu na ndiyo maana wenye wivu wanaumia.
"Wenye wivu wapo sana, hata Mungu aliumba malaika wakatokea mashetani humo humo, wakagoma, wakatupwa duniani, nao lazima wawe na wivu."
Akidhihirisha ni jinsi gani nchi inakwenda vizuri, Rais Magufuli alisema kipidi cha nyuma ilikuwa ni maajabu kwa Tanzania kuonekana angani lakini sasa hivi heshima yake imerudi.
"Ndege ndiyo heshima ya nchi, tumeingia (madarakani) na kuamua lazima tuwe na ndege zetu na tununue kwa fedha taslimu," alisema.
"Watu walijiuliza tutapata wapi fedha, nilisema nitawabana mafisadi watazitema tu na wamezitema na wasiozitema watazitema hata kwa kutapika."
Alisema zimenunuliwa ndege sita kwa mpigo bila kukopa kiasi cha dunia kushangaa na kwamba waliokuwa wanaongeaongea ndiyo wa kwanza kuzipanda.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani miezi 28 tu iliyopita, nchi ina ndege tatu mpya aina ya Bombadier Dash 8 Q400 huku tatu nyingine - Bombardier CS300 kutoka Canada na Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Marekani - zikitarajiwa kufika katikati ya mwaka.
"Tulitakiwa Watanzania tupendane bila kujali makabila, vyama; mafanikio haya tuyashangilie, nchi zilizostaarabika duniani masuala ya maendeleo wanaungana, ndege zikija siyo za familia ya Magufuli ni za Watanzania, tunajenga vituo vya rada kwa ajili ya Watanzania wote."
Aidha, Rais Magufuli alisema miradi yote ya maendeleo ni kwa ajili ya Watanzania na kwamba mawaziri wanapofanya juhudi kubwa, ikiwamo maboresho ya huduma za afya, huduma ya maji imeongezeka kwa asilimia 14.5 huku mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 11.5 hadi 17.5.
Aidha, alisema ujenzi wa rada za viwanja vya Dar es Salaam, Songwe, Zanzibar, Mwanza na Kilimanjaro, unatakiwa kukamilika kwa wakati kwa kuwa fedha zilishatengwa.
"Nakuagiza Waziri (wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa) kandarasi wa Mwanza asimamiwe ahakikishe jengo linakamilika," alisema Rais Magufuli.
"Suala la fedha serikali ya awamu ya tano haina tatizo na fedha, tena ulibadili mpangilio wa pa kuanzia, rada zote ziwekwe kwa pamoja."
Aidha, alimwagiza mkandarasi ahakikishe anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
"Waziri usiwe mpole. Nataka uonyeshe ukali wako, kama fedha ni tatizo sema hata leo (jana) utapelekewa, Katibu Mkuu yuko hapa peleka fedha. Asitafute kisingizio cha fedha, zimetengwa bilioni 67.5 kwa ajili ya kazi hii. Uwanja wa Mwanza umesuasua, nataka uwe wa kwanza kukamilika."
Awali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema mamlaka yake imedhamiria kuboresha sekta ya usafiri wa anga na kuchangia kikamilifu azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema mradi huo unatarajia kukamilika Mei mwakani ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya serikali na TCAA kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.
Hamza alisema mradi huo utasaidia kurahisisha huduma za utafutaji na uokoaji kunapotokea ajali za ndege, kuongeza mapato, kuongezeka kwa ndege, kuiwezesha nchi kukidhi viwango na miongozo ya Shirika la Kimatiafa la Usafiri wa Anga (ICAO) na kujenga imani ya watumiaji wa anga letu na kuendana na ushindani katika ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Alisema TCAA na Kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya Ufaransa wameingia makubaliano ya mradi huo ambao utagharimu Sh. bilioni 76.3 na serikali itachangia kwa asilimia 100.