Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC KIGOMA AANZISHA SHAMBA LA 'DHAHABU NYEUPE'...DC NDAGALA ACHEKELEA


Mkuu wa mkoa wa Kigoma brigedia jenerali mstaafu Emanuel Maganga ameanzisha shamba la pamba 'dhahabu nyeupe'  ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo wito uliotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kuhusu wananchi kujikita katika kilimo cha mazao ya kimkakati.

Akifanya zoezi la kunyunyizia dawa jana katika shamba lake katika kijiji cha Kanyonza, kata ya Kanyonza wilayani Kakonko, alilolima pamba hekari nne kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kulima zao hilo Maganga alisema wilaya ya Kakonko ndiyo wilaya waliyoiteua kwa ajili ya zao hilo.

Aliwaomba wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kulima ili kuweza kujiongezea kipato na kuinua uchumi wa wana Kakonko.

Alisema zao la pamba ni zao ambalo linaweza kuinua uchumi wa wakulima kwa haraka kwa kuwa zao hilo lina thamani kubwa sana na ni zao ambalo hata yeye amejitoa kulima ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha wananchi wanalima na kupata soko kwaajili ya kuuza zao hilo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema hivi sasa katika wilaya yake wakulima wamejitokeza kutoka wakulima 247 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 kufikia wakulima 1306 kwa mwaka 2017/2018 kutokana na uhamasishaji walioufanya na wakulima kupelekewa pembejeo za kilimo mapema.

Alisema maafisa ugani wamefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mashamba darasa, pamoja na kuhakikisha kila mkulima anapata dawa za viuwatilifu pamoja na kuwapa elimu ya namna ya kutunza zao hilo na kuhakikisha hawapati hasara.

Hata hivyo alisema changamoto iliyojitokeza mwanzoni ni dawa walizoletewa kutofanya kazi na wasambazaji wa dawa hizo baada ya kugundua tatizo hilo walilitatua na pamba inaendelea vizuri.

Aidha alisema matarajio ya zao hilo kwa mwaka huu ni kupata tani 1159.6 kutoka kwa wakulima 1306 waliolima hekari 1840 kutokana na wananchi kuitikia na usimamizi unaofanywa na maafisa ugani kwa ajili ya kuinua uzalishaji wa zao hilo.


Naye Mkulima na Mwezeshaji wa wakulima wa pamba Kata ya Kanyonza,Robson Banga alisema pamba imekuwa mkombozi kwa wakulima na ndiyo zao lililokuwa likiwaingizia fedha nyingi, mwaka uliopita walishindwa kulima kwa kuwa kulikuwa na upungufu wa mbegu na viuwatilifu kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kwa sasa wakulima wengi wamejitokeza kwa kuwa pembejeo zilifika kwa wakati.

Hata hivyo aliwashauri wakulima wenzake wajitahidi kulima pamba kwa kuwa pamba ni dhahabu nyeupe, na ni zao ambalo linaweza kuinua uchumi na wanapo jitokeza kwa wingi inasaidia sana serikali kuwekeza nguvu kubwa katika kuwekeza kwenye zao hilo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Kigoma brigedia jenerali mstaafu Emanuel Maganga akinyunyizia dawa kwenye shamba lake la pamba - Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Shamba la pamba la Mkuu wa mkoa wa Kigoma brigedia jenerali mstaafu Emanuel Maganga
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akinyunyizia dawa kwenye shamba la pamba

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com