Serikali imetoa mchanganuo wa Sh 1.5trilioni zinazodaiwa kutojulikana zilipo.
Akizungumza
bungeni leo Aprili 20, Naibu Waziri wa Fedha amesema kiasi cha Sh697
bilioni kilitumika katika matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva,
Sh 687bilioni kwa ajili ya mapato tarajiwa na Sh 203 bilioni ni za
mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar.
Kutolewa
kwa majibu hayo na Naibu Waziri, kulikuja baada ya Naibu Spika, Dk
Tulia Ackson kukatisha kipindi cha maswali na majibu na kuipa serikali
nafasi ya kutoa hoja ya kutoonekana kwa Sh 1.5 trilioni kwenye matumizi
ya Serikali.
Naibu Spika amesema bungeni hapo, maswali na majibu yatapangiwa utaratibu mwingine.
“Hakuna
Fedha kiasi cha Sh1.5trilioni iliyopotea au kutumika kwenye matumizi
ambayo hayakuidhinishwa na Bunge tukufu. Madai ya watu wasiyoitakia mema
nchi kuhusu matumizi ya fedha hii hawana nia njema na nchi,”amesema Dk
Kijaji
Amesema
kutoonekana kwa fedha hiyo kulitokana na taarifa ya ukaguzi ya CAG
kutumia taarifa za hesabu za nyaraka mbalimbali na hivyo kutojumuishwa
kwa baadhi ya taarifa za utekelezaji wa bajeti.
Amesema hadi kufikia Juni 2017, mapato yalikuwa Sh 25.3 trilioni na matumizi yalikuwa Sh23.79 trilioni.
“Matumizi haya hayakujumuisha Sh 697.85bilioni zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za serikali zilizoiva,” amesema
Hivi
karibuni, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alizungumza na
vyombo vya habari na kueleza kuwa katika ukurasa wa 34 wa ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali, (CAG)Sh 1.5 trilioni
hazikutolewa kwa matumizi wala kukaguliwa.
Social Plugin