Mtu aliyekula pilipili kali zaidi duniani katika shindano la kula pilipili kali alipelekwa hospitalini baada ya kuhisi maumivu makali ya kichwa.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 34 alikula pilipili aina ya Carolina Reaper katika shindano hilo lililofanyika mjini New York.
Maumivu hayo makali yalijiri baada ya siku chache.
Kisa chake kimechapishwa katika ripoti ya BMJ kwa kuwa ni kisa cha kwanza kuhusishwa na ulaji wa pilipili kali.
Daktari aliyesimamia kisa chake ameonya mtu yeyote anayekula pilipili kali kuelekea hospitalini iwapo atahisi maumivu yoyote ya kichwa.
Maumivu makali ya kichwa yanasababishwa na kukazwa kwa mishipa inayopeleka damu katika ubongo, tatizo linalojulikana kuwa cerebral vasoconstriction syndrome (RCSV).
Mara tu baada ya kula pilipili katika shindano hilo , mtu huyo alianza kuhisi kutapika. Alianza kuhisi maumivu makali katika shingo yake katika kipindi cha siku chache pamoja na kuumwa na kichwa, yakifanyika kila baada ya sekunde chache.
Maumivu hayo yalikuwa mabaya hadi akalazimika kuelekea katika chumba cha dharura hospitalini na kufanyiwa vipimo vya magonjwa kadhaa ya neva lakini matokeo yake yakawa mabaya.
Vipimo vya X-ray vilionyesha kwamba mishipa kadhaa katika ubongo wake ilikuwa imejipinda.
Kisa hicho ni cha kwanza kuhusishwa na ulaji wa pilipili. Awali ulaji wa pilipili aina ya Cayene ulihusishwa na kujipinda kwa mishipa ya moyo na kusababisha mshtuko wa moyo.
Dalili hupotea zenyewe. Na uchunguzi baada ya wiki tano ulibaini kwamba mishipa yake ya moyo ilirudi katika kiwango cha kawaida.
Ugonjwa huo kwa jina RCVS huisha baada ya siku chache ama hata wiki na muathiriwa huendelea kuchunguzwa na daktari, lakini katika visa vyengine mgonjwa hupatikana na kiharusi , lakini sio mara kwa mara.
Daktari Kulothungan Gunasekaran katika hospitali ya Ford mjini Detroit ambaye aliandika ripoti hiyo alisema kuwa watu wanafaa kujua kuhusu hatari wakati wanapokula pilipili.
''Hatutawashauri watu kula pilipili aina ya Carolina Reaper wakati huu, lakini tutapendekezea umma kuwa makini na athari na tunashauri kwamba wanafaa kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu wanapopatikana na maumivu bada ya kula pilipil kali.
Chanzo- BBC
Social Plugin