Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amekemea udhalilishwaji wa watoto ‘waliotelekezwa’ na baba zao ambao tangu jana picha zao zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii baada ya kufika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakiwa na mama zao.
Tangu jana wanawake waliotelekezwa na waume zao wamefika katika ofisi hizo zilizopo Ilala jijini hapa, kuanza kusikilizwa.
Katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter akijibu maoni ya wachangiaji, Dk Ndugulile alivionya vyombo vya habari kwa kushiriki kuonyesha picha za watoto katika mikusanyiko hiyo, huku akitaka utaratibu ufuatwe katika kusikiliza mashauri ya walalamikaji ikiwa ni pamoja na usiri.
“Ni kosa kisheria kwa chombo cha habari au mitandao ya jamii kuonyesha picha zenye kumdhalilisha mtoto kwa mujibu wa sheria ya mtoto Namba 21 ya 2009. Navikumbusha vyombo vya habari kulinda haki za watoto na kutokuwa washirika katika kudhalilisha haki za watoto,” alisema Dk Ndugulile kupitia ujumbe wa Twitter.
Akizungumza kwa njia ya simu na MCL Digital, Dk Ndugulile amekiri kuandika ujumbe huo na kusisitiza kufuatwa kwa utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya kijamii.
“Ushauri wangu kama Wizara inayosimamia haki za watoto, suala kama hili linapaswa kufanyika kwa faragha, kwa sababu una deal na watu na litakuwa endelevu,” amesema Dk Ndugulile.
“Anachokifanya Makonda ni jambo zuri, lakini linahitaji uangalifu na tufuate mifumo sahihi. Nitoe rai kwa wananchi wote kufuata taasisi zinazohusika.”
Alipoulizwa sababu ya wananchi wengi kujitokeza kwa mkuu wa mkoa kama ishara ya kuzidiwa kwa idara ya Ustawi wa Jamii, Dk Ndugulile alikanusha ,
“Si kwamba Ustawi wa Jamii umezidiwa, inawezekana wananchi hawana taarifa za kutosha kwa hiyo kupitia mikutano kama hiyo watapata taarifa. Tufuate mifumo rasmi inayokubalika kisheria,” amesema.
Na Elias Msuya, Mwananchi
Social Plugin