Mwanamke aitwaye Mugabe Ryoba (23) aliyeolewa Nyumbantobu katika kijiji cha Merenga wilayani Serengeti Mkoa wa Mara ameuawa kwa kukatwa na sime na mpenzi wake, Nchama Nchama (26) kutokana na wivu wa mapenzi.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea jana mchana Mei 28, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki amesema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa ametoroka.
“Matukio ya watu kuuana kwa silaha za jadi zimeshamiri lazima hatua zichukuliwe kudhibiti hali hii,”amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamieri, Dominick Kimoge amesema baada ya mwanaume kutoka kwenye shughuli zake, hakumkuta Mugabe nyumbani na baada ya muda aliwasiri na kuanza kumhoji akimtuhumu kuwa alikuwa kwa mwanaume mwingine.
Amesema alimshambulia kwa fimbo na mwisho akamkata kwa sime mkono wa kulia na kusababisha damu nyingi kuvuja na kumuacha ndani na kwenda kutafuta pikipiki ili kumpeleka zahanati.
Amesema mwanamke huyo alifariki dunia kabla ya kuanza kupata huduma ya kwanza, kwamba mtuhumiwa huyo ametokomea kusikojulikana.
Julius Magoiga mkazi wa kitongoji cha Mafyweko amesema “aliyekufa hakuwa mke wa mtuhumiwa kwa kuwa aliolewa na mama mmoja Ryoba Kibisa (nyumbantobu). Mtuhumiwa alikuwa ni kama dume la mbegu tu maana watoto wote wawili aliozaa hapo watakuwa wa mama aliyetoa mahari.”
Amebainisha kuwa kwa mila na desturi za Wakurya akina mama ambao hawakuzaa watoto wa kiume hulazimika kutafuta mwanamke na kumtolea mahari na anaweza kumchagulia mwanaume au atakayejitokeza akipata watoto hubaki kama wajukuu wa mji huo.
Na Anthony Mayunga, Mwananchi
Social Plugin