Mapenzi ni matamu, lakini yanapoingia dosari huweza kusababisha madhara na kufikia hatua hata ya waliopendana kuuana.
Matukio ya wanandoa kuuana yanaendelea kukithiri nchini na wanasaikolojia wametaja sababu kuu za visa hivyo kuwa ni usaliti, kunyimana unyumba, malezi ya wazazi na matumizi ya simu.
Pia wametaja sababu nyingine kuwa ni kukosekana upendo, hofu ya Mungu na masilahi.
Juzi muuguzi mfawidhi msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Rosemary Magombora (43) alipigwa na mumewe hadi kufariki na kisha mwili wake kufukiwa katika shimo lililo jirani na nyumba yao .
Tukio hilo lilitokea Kijiji cha Mkwalia, Tarafa ya Mkuranga.
Kaimu kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Rufiji, Mohamed Likwata alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Rosemary alipigwa Machi 21, kichwani na mumewe aliyetumia rungu.
Polisi wameeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mwanaume kudai kuwa mke wake alikuwa akimsaliti hadi ameambukiza Virusi vya Ukimwi (VVU).
Mwanaume huyo alikamatwa na polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Tukio jingine ni la usiku wa kuamkia jana Mei 26 wakati mhadhiri wa Kitengo cha Biashara katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Rose Mdenye kuuawa, huku mumewe akituhumiwa kuhusika na sababu zinazotajwa ni wivu wa mapenzi.
Ofisa uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Mtenga alisema jana kuwa Rose alikuwa mtumishi wa chuo hicho kikubwa nchini akifundisha masuala ya biashara.
Kamanda wa polisi wa Dodoma, Gilles Muroto alisema hakuwa na taarifa za tukio hilo kwa kuwa yupo nje ya mkoa.
“Nitakupa taarifa hizo kwa kina kesho (leo). Kwa sasa nipo Chamwino,” alisema.
Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya mkoa huo, Caroline Damian alisema waliupokea mwili wa Rose saa 5:00 usiku wa juzi.
“Mwili wake ulikuwa na majeraha mbalimbali ya visu. Alipokelewa akiwa ameshafariki,” alisema Caroline.
Alisema mwili wa Rose, aliyezaliwa mwaka 1987, ulitokea Swaswa mjini Dodoma.
Mume wa mhadhiri huyo anadaiwa kuwa ni mchungaji na mwalimu wa Chuo cha Biashara (CBE).
Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2017 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonyesha kuwa asilimia 16 ya matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yalisababishwa na wivu wa mapenzi.
Wanasaikolojia wanasemaje?
Mwanasaikolojia wa kampuni ya ushauri kwa wanandoa na familia ya Grace Inc, Grace Makani anasema chanzo cha mauaji hayo ni maendeleo wanayopata wanawake.
Grace anasema wanawake kwa sasa wanafanya kazi na biashara, hivyo wamejijengea hali ya kujiamini.
“Hilo bado wanaume hawajalikubali kwa hiyo inapotokea wakabishana kidogo kauli, mwanaume huhisi amedharaulika. Hasa mwanamke anapokuwa na kiburi akamjibu mume vibaya,” anasema.
Grace anasema tatizo jingine ni tofauti ya kihisia kati ya mwanamke na mwanaume unapotokea usaliti.
“Mwanamke anaweza kumfumania mume wake na akalia au akakasirika, baadaye akasamehe. Lakini mwanaume hawezi kusamehe. Ataona amedharaulika sana.”
Mtaalamu mwingine wa saikolojia na uhusiano, Dk Chris Mauki katika moja ya machapisho yake aliwahi kusema kuwa sababu za wanandoa kuuana ni usaliti, malezi ya wazazi, kunyimana unyumba, simu na masilahi.
Pia alisema kukosekana upendo miongoni mwa wanandoa na hofu ya Mungu ni sababu kuu.
Donansian Mang’on, mtaalamu mwingine wa saikolojia anayeishi Singida, anasema ujio wa simu umekuwa mwiba mwingine kwenye ndoa.
Anasema wapo baadhi ya wanandoa hawaaminiani na wamekuwa wakifuatiliana kwenye simu, jambo ambalo ni hatari na mwisho husababisha hasira na baadaye kupigana na mauaji.
“Utakuta mke anaamua kumfuatilia mumewe kwenye simu, kumbe mume ana mawasiliano na watu wengi wakiwamo wafanyakazi wenzake,” anasema.
“Anakuta ujumbe bila hata kuuliza ugomvi unaibuka na mwisho, watu wanaumizana na kuuana.”
Mwanasaikolojia huyo anasema wivu wa mapenzi ni sawa na chumvi ambayo isipokuwapo kwenye mboga hainogi na ikizidishwa chakula hakiliki.
Mang’on anasema kukosekana kwa hofu ya Mungu kwa baadhi ya wanandoa pia huchangia mauaji ndani ya ndoa.
Mtaalamu wa saikolojia mjini Tanga, Modesta Kimonga anasema mabadiliko ya kiuchumi yamewafanya wanaume kuwa na hasira.
“Ili kutafuta mbinu za kujihami, wamekuwa na hasira hata kuwadhuru wake zao. Kiakili hawako vizuri, hali hiyo inawaathiri,” anasema
Modesta anasema ile dhana ya mfumo dume bado inawaathiri wanaume hasa wanapoona wamekwama kiuchumi na wanawake kufanikiwa katika shughuli zao kama kushiriki vicoba.
Imeandaliwa na Julieth Ngarabali, Sharon Sauwa na Tumaini Msowoya - Mwananchi
Soma zaidi>>Wanandoa wengine wauana, wanasaikolojia wanena
Social Plugin