Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BODI YA PAMBA YATANGAZA BEI YA PAMBA MSIMU WA KILIMO 2018/2019

Bodi ya Pamba na wadau wa zao hilo wamekubaliana kuwa kilo moja ya pamba daraja A itauzwa kwa Sh 1,100 na pamba daraja B (pamba fifi) itauzwa kwa Sh 600 kwa msimu 2018/2019.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Kilimo, bei hiyo iliafikiwa katika mkutano wa pamoja wa wadau na Bodi ya Pamba uliofanyika Aprili 23.


Taarifa hiyo ilieleza kuwa bei ya pamba imepangwa baada ya kuzingatia vigezo vyote muhimu ambavyo ni kiwango cha kubadilishia fedha, bei ya pamba nyuzi, pamba ikiwa kiwandani, bei ya mbegu kwa wakamuaji wa mafuta ya kula.


Vigezo vingine ni kiwango cha uwiano wa pamba nyuzi na mbegu, faida ya wachambuaji, gharama za ununuzi, usafirishaji, ushuru wa halmashauri na mchango wa mfuko wa kuendeleza zao hilo.


“Februari 21, 2018 wadau wa pamba walikutana kwa uenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kukubaliana kubadili mfumo wa ununuzi wa zao hilo na kwamba pamba yote itanunuliwa kupitia vyama vya ushirika vya msingi.


“Utaratibu huu unaondoa mawakala wa makampuni binafsi kupima pamba ya wakulima na badala yale shughuli hiyo itafanywa na vyama vya ushirika vya msingi.


“Kampuni ya pamba ndiyo yatakayotoa fedha kwa ajili ya kununulia zao hilo,” ilisomeka taarifa hiyo.


Taarifa ilisema mfumo mpya wa ununuzi wa pamba una lengo la kuvifufua na kuviimarisha vyama vya ushirika kwa ajili ya kuwaunganisha wakulima na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani na pembejeo kwa wakulima wote wa pamba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com