Mbunge
wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo (CCM), amesema Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Luhaga Mpina ana mpango maalumu wa kuiondoa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), madarakani.
Akichangia
bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19, Bulembo amesema kama
operesheni sangara inayofanyika katika Ziwa Victoria ikiendelea CCM
itakuwa na wakati mgumu wa kuwaomba kura wananchi katika Uchaguzi Mkuu
na Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwakani.
“Kuna haja operesheni hiyo isimame ili kuwaokoa wavuvi ambao wanaathiriwa na operesheni hiyo,” amsema Bulembo.
Bulembo
amemwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kuunda Tume ya kwenda kuchunguza
operesheni hiyo kwani wavuvi wanaishi nchini kama watumwa.
“Wizara
hii kwa kweli tuna majonzi sana, nashukuru Mheshimiwa Spika umekaa hapo
mbele, ni vyema ukaunda tume ya Bunge kwenda kuangalia matatizo na
madhara yaliyowakuta wafugaji na wavuvi.”
Bulembo
akichangia kwa hisia amesema: “Wavuvi wa Tanzania wako katika utumwa
kwa sababu ukienda Ukerewe (anataja na visiwa mbalimbali) maisha yao ni
uvuvi, hawa watu leo ni kilio, si kilio kidogo ni kikubwa, watu
wamejinyonga, wamepigwa risasi.
“Wana
CCM wenzenu, tutakwenda kuomba kura, tutakwendaje kuomba kura,
haiwezekani utu wa mtu ukaharibika kwa sababu Mpina ni waziri, katika
hili tume haipukiki, CCM ni ya watu, Rais anaongelea wanyonge, wanyonge
wa Mafia, Mtwara, kanda ya ziwa.
“Mnakwendaje kuomba, Mtanzania anakuwa mtumwa, wafanyakazi wanalia, wakulima wanalia, itawezekanaje, Mpina huwatendei haki.”
Social Plugin