Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amewataka wananchi wilayani Kilindi, mkoani Tanga kutimiza wajibu na kufuata utaratibu wa kupata Mji Mdogo wilayani humo.
Waziri Jafo aliwataka wananchi hao ambao walikuwa wamebeba mabango wakimtaja Waziri Jafo kuwa wanahitaji kupatiwa miji midogo ya Kibirashi na Elerai kutimiza wajibu wao wasiwe kama mtu anayetaka mchumba wakati mahari hajatoa.
“Mnatakiwa kukaa kujadili suala zima la mamlaka ya mji mdogo, mlipeleke kikao cha maendeleo ya Kata, baadaye kwa madiwani, na kisha Kikao cha Ushauri cha Mkoa ndipo liwasikishwe kwangu.
“Fanyeni maamuzi kupitia vikao vya kisheria ili uweze kuhalalalisha maamuzi yenu kwa kuwachia mamlaka husika kumalizia.
“Hayo yote hamjafanya, hujatoa mahari, unataka mchumba maana yake nini?” amehoji Waziri Jafo huku akionyesha kuchukizwa na hali hiyo.
Waziri Jafo alikuwa katika mkutano wa pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi akiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutatua mgogoro wa mpaka baina ya wilaya hizo.
Mohamed Hamad - Mtanzania
Social Plugin