Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Mapinduzi, Dk Bashiru Ally amesema msimamo wake kuhusu mabadiliko ya Katiba utakuwa tofauti na ule aliokuwa nao awali kabla ya kuingia kwenye siasa na atafuata maelekezo ya Chama chake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa katibu mkuu, Abdulrahman Kinana, Dk Bashiru aliyekuwa akitetea mabadiliko ya Katiba amesema msimamo huo aliutoa kwa kuwa alikuwa huru.
"Leo nazungumza kama Katibu Mkuu, yaani swali lako lina majibu humo humo, ukiwa mchambuzi unachambua kweli kweli. Ukiwa msemaji wa chama unawasilisha yaliyoamuliwa kwenye vikao,"amesema Dk Bashiru.
Ameongeza kuwa “Msimamo wa Halmashauri Kuu ndio chombo kikuu kilichoniliteua na inaweza kunifukuza. Kwenye uchambuzi kule nisingeweza kufukuzwa. Hapa kama wewe unanitakia mema, siwezi kuchambua yale ambayo hayajaamuliwa na vikao” amesema Bashiru
Dkt. Bashiru amekuwa akijihusisha katika shughuli zilizoratibiwa na Taasisi kwa muda mrefu pia alikuwa kinara katika zoezi zima la kudai mchakato wa Katiba mpya.