Kocha mpya wa Yanga mzaliwa wa DR Congo, Zahera Mwinyi, baada ya kufanya tathmini dhidi ya Simba amewaahidi mashabiki kwamba anakuja na mbinu mbadala ili kikosi chake ili kisifungwe tena kirahisi.
Jumapili iliyopita, Yanga ilifungwa bao 1-0 na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zitakutana tena msimu ujao kwani awali walitoka sare ya bao 1-1 katika ligi hiyo.
Mwinyi aliyeletwa Yanga kuchukua nafasi ya Kocha George Lwandamina aliyejiunga na Zesco United ya kwao Zambia, Jumapili iliyopita aliushuhusia mchezo huo akiwa jukwaani kwani hakua na vibali vya kufanya kazi nchini.
Mwinyi alisema ; “Nafurahi kuona mchezo wa Simba dhidi ya timu yangu ya Yanga, limekuwa ni jambo zuri sana kwangu kwani limenipa changamoto kubwa na limenifanya kuwajua mapema wapinzani wangu hasa nitakapoanza kufundisha rasmi.”
“Yanga ina wachezaji wazuri sana sema kuna mambo machache tu ambayo nitakapoyafanyia kazi kikosi changu kitakuwa imara zaidi kisichofungika kirahisi kwani siyo kibaya kama ambavyo nilikuwa nikiambiwa.
“Kikosi kingekuwa kibaya kwa mchezo ule wa Jumapili tungefungwa mabao mengi sana ila kwa kuwa wapo safi utaona walipambana vya kutosha na hata lile bao yalikuwa na makosa kidogo tu ya uwanjani,” alisema Mwinyi ambaye amewahi kufundisha Ubelgiji.