MAHAKAMA YAIKABA SERIKALI KESI YA MHASIBU WA TAKUKURU

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha kuchapa maelezo ya washtakiwa wa kesi ya kumiliki mali zisizoendana na kipato, inayomkabili mhasibu mkuu wa Taasisi na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera na wote wanakabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji wa fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.

Uamuzi huo umetolewa leo Mei 16, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kesi hiyo kuahirishwa kwa zaidi ya mara saba,ikiwa katika hatua ya kuwasomea hoja za awali (PH), washtakiwa hao.

Hatua hiyo, inatokana na upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa wapo katika hatua za mwisho za kuchapa maelezo ya washtakiwa.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, lakini walikuwa hawajakamilisha uchapaji wa maelezo ya washtakiwa hao.

“Kesi imekuja kwa ajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wote , lakini tunaiomba Mahakama itupe ahirisho la mwisho ili tuweze kukamilisha uchapaji wa maelezo ya washtakiwa,” amedai wakili Peter.

“Tayari maelezo ya washtakiwa tumeshaanda na kilichobaki ni kuchapwa tu, hivyo tunaiomba Mahakama yako itupe ahirisho la mwisho.”

Baada ya maelezo hayo, wakili wa utetezi, Semi Malimi na Alex Mgongolwa wamedai kuwa maelezo ya awali yameahirishwa kusomwa kwa zaidi ya mara saba kuanzia April 4, 2018.

Baada ya kupitia maelezo ya pande zote, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, 2018 na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha kuchapa maelezo hayo ili washtakiwa hao waweze kusomewa maelezo ya awali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post