Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya firauni! Ndivyo unavyoweza kusema kwa mama huyu wa wato wawili anayefahamika kama Mama Theresia (18), mkazi wa Kata Maweni, Mtaa wa Jaribu Tena, jijini Tanga ambaye huwang’ata watoto wake kisha kuomba radhi kwa mumewe.
Hali hiyo imemfanya mume wake, Patrick Peter (75) kuomba msaada kwa wasamaria wema na serikali kumsaidia kuwachukua watoto wake wawili ambao wako hatarini kutokana na mama yao kuwafanyia vitendo vya ukatili.
Aidha, Mzee huyo amesema mke wake huyo waliyedumu kwa miaka mitano hupandisha hasira na kufanya matukio yasiyo ya kawaida na baadaye kuomba radhi.
Akisimulia mikasa hiyo ya mkewe, Mzee Parick amesema mama huyo amekuwa akifanya vitendo vya ukatili kwa watoto hao kwa kuwang’ata na meno na kuwasababishia majeraha makubwa mwilini.
“Hata mimi amewahi kunishikia panga akataka kunipiga nalo, ila niliwahi kumshika, hivyo unaweza kuona namna gani mama huyu amekuwa tishio kwa familia,” amesema.
Kwa upande wao majirani wa Mama Theresia, wameshangazwa na vitendo vya mama huyo na kuomba serikali kuwapatia msaada watoto hao kwa kuwahamisha kutokana na maisha hatarishi wanayoishi na wazazi wao.
“Sisi tulikwenda kujumuika msibani hapo kwa Mzee Patrick aliyefiwa na mtoto wao mchanga, baada ya kumaliza shughuli za mazishi ndiyo ndugu mmoja akasema jamani humu ndani pia kuna kabinti kadogo kana majeraha makubwa mwilini na amedhoofika sana anaweza kupoteza maisha tusipochukua hatua,” amesema mmoja wa majirani.
Hata hivyo, mtoto huyo wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitano, ameonekana kudhoofika kutokana na vidonda vikubwa vinavyoonekana dhahiri ni alama za meno.
Aidha, mtoto huyo aliyefariki Jumanne wiki hii, imedaiwa kifo chake kilisababishwa na mama huyo kumpa uji mwingi uliosababisha mtoto huyo wa wiki mbili kuvimbiwa na kupoteza maisha.
Akizungumzia suala hilo, Mama Theresia mwenyewe amekana kuwangata watoto wake na kwamba amedai huwa wanaanguka wanapojifunza kutambaa hatua inayowasababishia kupata majeraha hayo.
Susan Uhinga- Mtanzania Tanga
Social Plugin