Na Rhoda Ezeikel - Malunde1 blog Kigoma
Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Kakonko wilayani Kakonko mkoani Kigoma Dr. Mejo Banikila (43) amekutwa amejiua kwa kujinyonga chumbani kwake kwa kutumia taulo.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Mei 29,2018.
Kwa mujibu wa wapangaji wenzake na marehemu wameeleza kuwa kwa muda wa miezi nane wameishi naye vizuri licha ya kuwa siku mbili kabla ya tukio amekuwa akionekana mnyonge mpaka tukio hilo lilipotokea.
Wamesema Mganga huyo alikuwa akifanya kazi zake vizuri na amekuwa akijitoa sana kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati na kwamba watamkumbuka kwa mambo mengi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalamawilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo aliyefika nyumbani kwa marehemu huyo amesema matukio ya watu kujinyonga katika wilaya ya Kakonko yamekuwa yakiongezeka na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini nini hasa sababu za watu kuchukua maamuzi magumu kama hayo.
Kanali Ndagala amewataka wananchi kuhudhuria kanisani na misikitini ili kusikiliza mahubiri na kupunguza msongo wa mawazo kwa kuwaeleza wenzao ili waweze kuwashauri na kuepukana na tatizo hilo la wananchi kujinyonga.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kigoma Martin Otieno amethibitisha kutokea tukio hilo na kuwaomba wananchi kuacha kuchukua maamuzi ya kujinyonga kwa sababu yeyote ile kwa kuwa ni matukio ambayo yameendelea kutokea nchini na kwamba wanaendelea na uchunguzi kujua sababu iliyosababisha mganga huyo kuchukua maamuzi hayo.
Social Plugin