Gavana wa Mji Mkuu wa Kenya Nairobi Mike Mbuvi Sonko amependekeza mwanasaisa wa upinzani anayekumbwa na utata Miguna Miguna kuwa Naibu Gavana.
Sonko ametoa tangazo hilo ambalo halikutarajiwa siku ya (jana) Jumatano jioni kwa njia ya barua kwa Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi, akisema Miguna Miguna ametimiza matakwa yote yanayohitajika kikatiba.
Barua hiyo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua maoni mengi kutoka kwa Wakenya, kutokana na kuwa uteuzi wake umekuja wakati ambao haukutarajiwa kwa kuwa Bw Miguna amekuwa mkosoaji mkuu wa Gavana huyo na kabla ya uchaguzi kwa kudai Sonko hana sifa zozote za uongozi na hawezi kuongoza jiji la Nairobi.
Miguna alitarajiwa kurudi nchini Kenya siku ya jana kutoka Canada baada ya kutimuliwa na serikali, lakini akaahirisha safari yake akisema kuwa idara ya uhamiaji huikumpa pasipoti halali jinsi ilivyoagizwa na mahakama.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amesema Bw. Miguna atahitajika kutatua masuala kuhusu uraia wake na serikali ya Kenya kabla ya kuhojiwa na wabunge wa jimbo hilo.
Bw Miguna anahitaji kuidhinishwa na bunge hilo kabla ya kuchukua wadhifa huo.
Hata hivyo Miguna mpaka sasa bado hajazungumzia chochote kuhusu barua hiyo.