Victoria Salvatory (58), mkazi wa kata ya Katoma, Kagera anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mumewe, Salvatory Iteganira (62) kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi amesema mauaji hayo yalitokea jana saa 6:00 mchana.
Akizungumza leo Mei 28, Kamanda Ollomi amesema mtuhumiwa anadaiwa kumpiga mumewe kwa kitu kizito kichwani na kumsababishia jeraha lililovuja damu nyingi na hatimaye kifo.
“Wanandoa hao wanadaiwa kuwa na ugomvi ambao chanzo chake tunaendelea kuchunguza; baada ya ugomvi huo mtuhumiwa alimpiga mume wake kichwani kwa kitu kizito kilichosababisha jeraha lililovuja damu nyingi na kusababisha kifo chake,” amesema Ollomi.
Kamanda huyo amewaasa wanandoa na wapenzi kutumia njia ya majadiliano, usuluhishi na sheria kutatua tofauti miongoni mwao badala ya kujichukulia sheria mikononi.
Matukio ya hivi karibuni ya mauaji ya wanandoa ni pamoja na la Muuguzi mfawidhi msaidizi wa hospitali ya wilaya ya Mkuranga, Rosemary Magombora (43), anayedaiwa kuuawa na mume wake kisha kufukiwa shimoni.
Tukio jingine ni la mhadhiri wa kompyuta wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Rose Mdenye anayedaiwa kuuawa na mume wake, John Mwaikambo.
Na Alodia Dominick, Mwananchi
Social Plugin