Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA AMUWEKA MAHABUSU MWENYEKITI WA CCM


 Mgogoro unafukuta wilayani Mwanga ambako mkuu wa wilaya hiyo, Aaron Mbogho anadaiwa kumuweka mahabusu mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Jaffary Kandege.


Kwa kawaida kiongozi wa CCM kwa ngazi kama hiyo, anatakiwa kuwa juu ya kiongozi nwa Serikali kutokana na chama hicho kuwa kimeshika Serikali.


Lakini mkuu huyo wa wilaya aliagiza apelekwe kituo cha polisi.


Taarifa zinadai kuwa mwenyekiti huyo wa CCM aliwekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mwanga Ijumaa wiki iliyopita kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 8:00 usiku kabla ya kudhaminiwa na diwani wa Shighatini (CCM), Enea Mrutu.


Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti huyo alisema kwa hali ya mgogoro huo ilipofikia, hayupo tayari kufanya kazi na DC huyo kwa kuwa amekidhalilisha chama na yeye binafsi.


Tukio la kukamatwa kwa Kandege limekuja wiki moja tangu kikao cha baraza la madiwani wa wilaya kidai kuwa hawana imani na mku huyo wa wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama.


Kauli ya madiwani hao ilitokana na kuendelea kukithiri kwa uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, huku baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi na maofisa maliasili wakinyooshewa kidole kwa kukosa uadilifu.




DC atema cheche


Hata hivyo, DC Mbogho amedai Kandege hakufikishwa polisi na kuhojiwa kwa wadhifa wake wa mwenyekiti wa CCM wa wilaya.


“Muulizeni aliandikisha maelezo kuhusu tuhuma gani? Ukipelekwa mahabusu kwa amri ya DC huwa huandiki maelezo ya kijinai. Hajahojiwa kama mwenyekiti wa CCM, bali Jaffary Kandege,” alidai Mbogho.


Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya kama kosa analotuhumiwa nalo, lingekuwa linahusu wadhifa wake wa uenyekiti wa CCM wilaya, lingeshughulikiwa kwa mujibu taratibu za kichama.


Mbogho alidai kuwa wao kama kamati ya ulinzi na usalama walipokea taarifa kuwa Kandege anahusishwa na tuhuma za kushawishi wananchi kuwashambulia maofisa na magari ya Serikali.


“Alipelekwa pale kwa tuhuma za uchochezi na alipokuja ofisini kwangu nilimwambia waziwazi kuwa unatajwa katika hili na itabidi ukaandike maelezo polisi. Wala hakuwekwa kwa saa 48,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.


“Huyo mtu ana matatizo yake binafsi asiyafiche kwenye chama changu. Umma utenganishe mtu na wadhifa. Mhalifu atabaki kuwa mhalifu tu na sheria itachukua mkondo wake bila uonevu.”


Mkuu huyo wa wilaya alisema ni utaratibu ulio wazi kuwa mshukiwa wa uhalifu ni lazima ahojiwe na kudhaminiwa, na kwamba Kandege huenda alikaa polisi kwa muda huo akisubiri kudhaminiwa.


Alidai kumekuwapo na matukio ya maofisa wa maliasili na polisi wanaokwenda kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kushambuliwa kwa mawe na baadhi ya wananchi.




Malalamiko ya Kandege


Hata hivyo, Kandege aliiambia Mwananchi kuwa kitendo cha kuwekwa mahabusu kinatokana na chama kumtaka DC Mbogho awape taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM.


“Nilipowekwa mahabusu tumetafakari sana na wenzangu ndani ya CCM na kujiuliza kulikoni? Tatizo nini? Tukajiuliza labda ni kwa sababu tumemtaka atuletee taarifa ya utekelezaji wa ilani,” alisema.


“Ameona afanye hivyo ili kunipunguza nguvu, lakini nitaendelea kupaza sauti pale ambapo naona mambo hayaendi sawa. Kila tukimtaka kwenye kamati ya siasa alete taarifa, haleti.


“Tabia ya kuwawekaweka watu ndani ikome kwa sababu si nzuri. Ameshawaweka mahabusu watendaji wengine wa Serikali. U-DC isiwe ndio fimbo ya kuwatandika watendaji wa Serikali.”


Mwenyekiti huyo alisema mwezi Januari, mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alifanya mkutano katika kitongoji cha National uliohudhuriwa pia na mkuu huyo wa wilaya.


“Kwenye ule mkutano wananchi walilalamika kuwa baadhi ya polisi na maofisa maliasili wanapokamata makokoro, wanachukua fedha nyingi na kuachia makokoro,” alisema Kandege.


“Kwanza nilikemea vikali tabia ya wananchi kupiga mawe watendaji wa Serikali wanapotekeleza majukumu yao, lakini nikawataka polisi na maofisa maliasili wanaolalamikiwa nao wawe waadilifu.


“Vyombo vyote vya ulinzi na usalama mkoa na wilaya vilikuwapo na nilisema kwa ujumla wake. Nashangaa leo kuitwa na kuhojiwa na kubambikiwa kesi ya uongo ya kushambulia gari la polisi.”


Mwenyekiti huyo alidai mkuu huyo wa wilaya ana mgogoro na kamati ya siasa ya wilaya, kwa vile kila anapopelekewa barua ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani, hafanyi hivyo.




RPC, katibu wa CCM wanena


Kamanda wa polisi wa mkoa, Hamis Issah hakutaka kuzungumzia suala hilo na kuelekeza atafutwe mkuu wa Wilaya ya Mwanga kwa kuwa ana mamlaka ya kulizungumzia.


Lakini katibu wa CCM wa wilaya, Mwanaidi Mbisha alisema wanashughulikia suala hilo ndani ya chama.


“Jambo hili ni la kichama. Tunalishughulikia wenyewe (CCM) kwa hiyo mliache kama lilivyo,” alieleza Mbisha.




Viongozi, wana CCM wafunguka


Viongozi wa kisiasa na baadhi ya wanachama wa CCM waliohojiwa na Mwananchi, walidai kushtushwa na kitendo cha DC huyo na kutaka chama kiingilie kati.


“Kiukweli mimi naona kuna visa fulani na moja ni hili la madiwani kumkataa DC. Labda anaona chama kina mkono wake. Yule (Kandege) ni kiongozi, haikuwa busara kumuweka mahabusu,” alisema diwani wa Shighatini (CCM), Mrutu aliyemdhamini mwenyekiti wake.


Mrutu alisema anachofahamu ni kuwa katibu wa CCM wa wilaya hiyo ameshaagizwa kuitisha kikao cha halmashauri ya wilaya ili kujadili suala hilo ambalo alidai limewaudhi wanachama, na kisha kutoa msimamo wa chama.


Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kijiji cha Ruru (CCM), Juma Rehani alisema kuwa hawaridhishwi na utendaji wa mkuu huyo wa wilaya na ndio maana walitishia kuhamia nchi jirani ya Kenya.




Das alivyoswekwa mahabusu


Hii si mara ya kwanza kwa DC Mbogho kutuhumiwa kuamuru viongozi kusekwa ndani.


Inadaiwa kuwa Agosti 10, 2017, mkuu huyo wa wilaya aliamuru kuwekwa mahabusu kwa katibu tawala wake (Das), Yusuph Kasuka, lakini DC akasema hakuwekwa ndani kwa sababu ya wadhifa wake, bali kama Kasuka.


Kasuka alikaririwa na Mwananchi akisema hafahamu sababu wala kiini cha kukamatwa bali polisi walifika ofisini kwake kumchukua na kutaka sababu za kukamatwa kwake aulizwe mkuu wa wilaya.


Lakini taarifa zilidai baadaye kuwa DC aliamua kuchukua uamuzi wa kulipeleka suala la Das wake polisi baada ya kunusa harufu ya ufisadi katika matengenezo ya gari mojawapo la ofisi yake.
CHANZO-MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com