Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela amefungua mafunzo kwa wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Shinyanga yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kupiga vita ukatili katika jamii.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza leo Jumatano Mei 30,2018 yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga yamekutanisha wadau mbalimbali wanaohusika katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Investing in Children and their Societies (ICS – Africa).
Awali akizungumza,Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga Glory Mbia alisema lengo la mafunzo hayo ni kupata maoni na mapendekezo mbalimbali katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Lengo la mafunzo haya ni kupata uelewa wa pamoja na kutengeneza mkakati namna gani tunafanya katika kutokomeza vitendo vya kikatili katika mkoa”,alisema Mbia.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo alisema mkoa wa Shinyanga bado una tatizo kubwa la ukatili dhidi ya watoto na wanawake hivyo zinahitajika nguvu za pamoja
“Tunamshukuru mwenyezi Mungu mauaji dhidi ya albino yamebaki historia katika mkoa wetu,lakini katika jamii kumekuwa na unyanyasaji hasa wa watoto,kupitia kamati hii naamini kwa pamoja kama tutaamua kwenda pamoja hatua kwa hatua tutaweza kutokomeza vitendo vya ukatili katika mkoa huu”,alieleza Msovela.
“Akina mama na watoto wengi wameathirika kisaikolojia,kimwili,wapo watoto wamekosa elimu kutokana na unyanyasaji wanaopitia kwa pamoja naamini sheria ambazo zipo na umoja huu tutaweza kukabiliana na ukatili wanaofanyiwa wanawake na watoto”,alisema.
“Kwa namna ya pekee niwashukuru sana wadau wetu wa maendeleo ICS ambao wamejitolea kudhamini mafunzo haya,na hivi sasa kamati imeshaundwa kutoka katika ngazi ya kata,halmashauri na sasa tunaendelea na mafunzo kwa ngazi ya mkoa”,aliongeza Msovela.
Kwa upande wake,Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule alisema umaskini umekuwa chanzo cha vitendo ukatili dhidi ya wanawake hivyo ili kutokomeza vitendo hivyo ni vyema wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi huku wadau wote wakiweka nguvu pamoja katika kuwalinda na kuwatetea wanawake na watoto.
Naye Meneja wa shirika la ICS nchini,Kudely Sokoine Joram alisema ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,shirika hilo limekuwa likishirikiana na serikali ili kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa salama katika jamii.
“Kupitia mradi wetu wa masuala ya ulinzi na usalama wa watoto tunafanya mradi huu katika manispaa ya Shinyanga,Shinyanga Vijijini na wilaya ya Kishapu na baada ya serikali kumaliza kutengeneza mwongozo,ilituomba tunapokuwa na rasilimali basi tuweze kusaidia serikali kuhakikisha kamati zinaundwa na zinapata mafunzo ndiyo maana hata haya mafunzo tumeyawezesha sisi”,alieleza.
Meneja huyo wa ICS alisema katika ngazi ya halmashauri,kata na vijiji mpaka sasa wamezisaidia kamati 25 wakishirikiana na serikali na wanaendelea kuwezesha uundwaji wa kamati ili kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Sisi kama wadau wa maendeleo tunashughulika na masuala ya malezi na matunzo bora ya watoto,masuala ya ulinzi wa watoto kwa mfano miongozo ya serikali na sheria zilizopo lakini pia kuwezesha familia katika masuala ya kiuchumi,kujenga uwezo wa taasisi ndogo ndogo na maeneo husika yanayoshughulika na maendeleo ya jamii”,alisema Joram.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akifungua mafunzo ya kujengea uwezo kwa wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Shinyanga leo Mei 30,2018 - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akifungua mafunzo na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga Glory Mbia akielezea malengo ya mafunzo hayo ambapo alisema lengoni kupata maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu namna ya kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Meneja wa shirika la ICS nchini Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema wameamua kufadhili mafunzo hayo ili kushirikiana na serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Meneja wa shirika la ICS nchini Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza ukumbini.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon akielezea namna wanavyoshiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga.
Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule akielezea Muhtasari kuhusu Mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada ukumbini.
Mafunzo yanaendelea.
Kushoto ni Afisa Maendeleo Mwandamizi, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mathias Haule na Afisa Mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kutoka shirika la ICS mkoa wa Shinyanga,Shadia Nurdin wakiangalia nyaraka zinahusu masuala ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin