Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo amefanya ziara ya kushtukiza bandarini jijini Dar es salaam kukagua matanki ya mafuta ya kula, ambayo yameadimika hapa nchini.
Baada ya ziara hiyo na kufanya ukaguzi, Rais Magufuli amebaini kuwa kuna mafuta ambayo yameingizwa nchini huku kukiwa na taarifa za udanganyifu ili kukwepa kodi, yakiwemo mafuta ambayo yameshakamilika (refined oil) na kusema kuwa ni mafuta ghafi (crude oil).
Baada ya kugundua hilo Rais Magufuli amewataka wamiliki wa mafuta hayo kulipa ushuru wake unaostahili, pamoja na faini kutokana na udanganyifu walioufanya.
"Kwenye bidhaa walizosema ni crude kumbe ni refined oil walipe 25% pamoja na fine, hatuwezi tukawa tunaibiwa kila siku tunahitaji kujenga viwanda vetu, haiwezekani crude oil ukachaji sawa na semi refined, na hii sheria yetu inawezekana kulifanyika mchezo, wabunge walipitisha kitu kingine, kinachojadiliwa kingine, kilicholetwa huku ni kingine, kinachokuja kupitishwa kuwa sheria kimebadilishwa kuwa kingine, "Hii crude oil ichajiwe bei ya juu ili watu wengi wajenge viwanda hapa ili tujenge nchi yetu ”, amesema Rais Magufuli.
Sambamba na hilo Rais Magufuli amemtaka mkemia Mkuu wa Serikali kufuata maadili ya kazi, ili kuleta weledi na kujenga nchi.
"Mkemia Mkuu nataka sampo zozote mtakazokuwa mnapewa fanyeni kwa utaratibu kwa kuzingatia maadili, mkiletewa mkono wa albino semeni mkono wa albino msije mkasema mkono wa mbwa. Mkiletewa madawa ya kulevya semeni haya ni madawa ya kulevya sio unga wa muhogo, amesema Rais Magufuli.