Shirikisho la soka nchini TFF leo Mei 16, limethibitisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi na kukabidhi vikombe vya ubingwa wa Serengeti Boys na Simba.
Mtendaji mkuu wa TFF Wilfred Kidao amesema wamethibitishiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuwa Rais Magufuli amekubali kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa Simba SC dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi hii.
''Rais Magufuli amekubali ombi la TFF kuwakabidhi vijana wa Serengeti Boys Kombe la CECAFA waliloshinda hivi karibuni nchini Burundi, tukio ambalo litaambatana pia na kuikabidhi Simba SC kombe la ubingwa wa VPL msimu huu'', amesema.
Serengeti Boys wameibuka mabingwa wa soka katika ukanda wa Africa Mashariki na Kati baada ya kutwaa ubingwa huo kwa kuwafunga vijana wa Somalia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali.
Simba imetwaa ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2017/18 baada ya kufikisha alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kati ya 16 za ligi kuu msimu huu.
Social Plugin