Kiungo
wa zamani wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango kesho Alhamisi anatimiza
miaka sita kaburini katika wiki ambayo Simba inabeba kombe jingine tangu
yeye afariki.
Simba
haikuwahi kubeba Kombe la Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2012 ambao
Mafisango alikuwa kikosini na kupachika mabao 12 akicheza kama kiraka.
Simba
ambayo msimu huu imetwaa ubingwa bila kupoteza mchezo itakabidhiwa
kombe lake Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mechi dhidi ya
Kagera Sugar ya kipa Juma Kaseja ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa
Mafisango.
Jumapili
hiyo itakuwa Mei 20, ambayo ndiyo siku ambayo Mafisango aliyefariki
Mei 17 mwaka 2012, alizikwa majira ya saa 11 jioni kwenye makaburi ya
Lemba, nje kidogo ya Jiji la Kinshasa. Hivyo Simba wakati wakijiandaa
kubeba Kombe lao mida hiyo ya jioni Mafisango atakuwa akitimiza miaka
sita ndani ya kaburi pale Kinshasa.
Mafisango
ambaye alikuwa na uraia wa DR Congo na Rwanda, alifariki kwa ajali ya
gari iliyotokea eneo la Keko jijini Dar es Salaam wakati akitokea kwenye
starehe kurejea nyumbani kwake tayari kwa safari ya kurudi kwao Rwanda
kujiunga na kambi ya timu ya Taifa.
Moja
ya vitu ambavyo vilishangaza Watanzania wengi kwenye maziko ya
mchezaji huyo ni staili ya washikaji zake kupitisha jeneza lake kwenye
vijiwe vyake vyote kuaga ndugu na rafiki zake ikiwemo Baa kabla ya
kuunganisha makaburini.