Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata malori mawili yenye bidhaa mbalimbali eneo la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kupitia njia ya magendo yakitokea nchini Kenya zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20
Akizungumza jana jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere alisema kuwa, malori hayo yenye namba T 985 AJP na T 840 ABF yalikamatwa usiku wa tarehe 10 Mei, 2018 na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo wamevunja sheria kwa kuwa hawakulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.
Kichere alifafanua kuwa, wafanyabiashara wenye bidhaa hizi zilizokamatwa, wamevunja kifungu cha sheria namba 82 na 200 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 na Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004.
"Kwa ujumla bidhaa hizi zote zina thamani ya shilingi 20,037,330.15 ambayo kodi ya bidhaa hizi ni shillingi 28,524,758.11 na adhabu au faini ya bidhaa hizi ni shilingi 10,768,665.08. Hivyo jumla ya mapato
yanayotakiwa kulipwa Serikalini ni shilingi 39,293,423.19," Kichere.
Ameongeza kuwa "Hivyo kwa Sheria hizo, wafanyabiashara hawa wanatakiwa kulipa kodi pamoja na faini ya shilingi milioni 39 na magari yao kutaifishwa".
Amezitaja bidhaa zilizokamatwa kuwa ni pamoja na mifuko 362 ya sukari yenye uzito wa kilo 50 kila mmoja, maboksi 40 ya mafuta ya kula yanayoitwa Karibu, maboksi matatu ya mafuta ya kula yanayoitwa Daria, magaloni 100 ya mafuta ya kula yanayoitwa Nyata na maboksi matatu ya viungo vya mboga
Kufuatia tukio hilo, Kamishna Mkuu Kichere amewakumbusha wafanyabiashara wote kuzingatia taratibu za uingizaji bidhaa nchini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na kuongeza kuwa, TRA haitavumilia ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara kwa kutozingatia sheria na taratibu hizo.