Mamlaka
ya Mapato (TRA), imetangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Paul
Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa atashindwa kuzilipia
ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu.
Kontena
hizo za Makonda ambazo zimesubiri utaratibu wa kuzitoa TRA kwa zaidi ya
siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi, zimesheheni samani
za ndani na ofisini.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, jana alisema
kuwa kwa kawaida bidhaa zote zinapoagizwa na kufika bandarini
zinatakiwa kuondolewa ndani ya siku 90.
Kayombo
alisema inapotokea muda huo ukapita bila wahusika kuondoa mizigo yao,
hujulishwa na mamlaka hiyo kwa kupewa notisi ya siku 30 ili waondoe.
Kwa
mujibu wa tangazo la TRA lililotoka kwenye vyombo vya habari Jumatatu,
Mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa wateja nane akiwamo "Paul
Makonda" ambao mizigo yao imekaa bandarini zaidi ya muda unaotakiwa.
Katika
tangazo hilo, Kamishna wa Idara ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa,
ametoa siku 30 kwa wamiliki wa mali mbalimbali zilizopo katika ghala la
TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya muda huo zitapigwa mnada kwa
mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa forodha.
Kayombo
alisema kuwa, mzigo unapopitiliza muda wa kukaa bandarini, TRA
huwakumbusha wahusika kwa kuwapa notisi kama ya siku hiyo.
"Tumetoa
tangazo hili ili kontena ambazo ziko bandarini ambazo zimepitiliza siku
90 wahusika waende kuziondoa; wasipotekeleza ndani ya muda tuliowapa
tutazipiga mnada kwa mujibu wa sheria," alisema.
Kayombo alisema nyaraka za bidhaa hizo ziko sawa tatizo ni muda wa kuziondoa bandarini hapo ndiyo haujafuatwa.
"Siwezi
kusema kama wameshindwa kulipa kodi au la lakini hata ikitokea bidhaa
ambazo zina msamaha wa kodi zimekaa zaidi ya siku zilizowekwa na
wamiliki wakapewa notisi bila kutekeleza, muda wa notisi ukiisha bidhaa
husika hupigwa mnada na kwenye hili hatuangalii bidhaa zimetoka wapi, ni
msaada au sio msaada," alisema Kayombo.
"Bidhaa
ikipitiliza siku za kukaa bandarini kwa mujibu wa taratibu, tunatangaza
bila kuangalia zimeagizwa na nani, kuna nini ndani yake, zimelipiwa ama
hazijalipiwa kama hazijaondolewa bandarini, tunatangaza, ndivyo
tulivyofanya."