Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Venance Mabeyo.
**
BUNGE limeanika majina ya taasisi za serikali zinazodaiwa mabilioni ya shilingi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma jana taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka ujao wa fedha, mjumbe wa kamati hiyo, Joram Hongoli, alisema wadaiwa sugu hao ni pamoja na wizara nne na halmashauri tatu.
Alizitaja taasisi hizo ambazo kwa pamoja zinadaiwa na jeshi zaidi ya Sh. bilioni 40 kuwa ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Fedha na Mipango.
Nyingine ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Dar es Salaam, Chuo cha Madini - Nzega, Stamigold - Biharamuro na Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo na Halmashauri za Wilaya za Kasulu, Kibaha na Geita.
Akifafanua kuhusu madeni hayo, Hongoli alisema halmashauri hizo tatu ni miongoni mwa wadaiwa sugu waliokopa matrekta kutoka Suma JKT ambao mpaka sasa deni lao limefikia Sh. bilioni 40.
Alisema wizara nne ni sehemu ya wadaiwa wa SUMA JKT Guard Ltd, akibainisha kuwa hadi Mei mwaka huu, deni lililokuwa limelipwa ni Sh. bilioni 3.451 kati ya Sh. bilioni 4.057.
SERA YA ULINZI
Hongoli pia alisema kamati yao inaishauri serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, kuwasilisha haraka maoni ya upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu rasimu ya Sera ya Ulinzi, ili kukamilisha sera hiyo kwa kuwa mchakato huo kwa sasa unasubiri maoni hayo.
Alisema uwapo wa sera hiyo utawezesha marekebisho ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya Mwaka 1966, Sura 192 ili iendane na wakati, mifumo ya utawala na mahitaji ya kisasa ya kisheria katika sekta ya ulinzi.
Vilevile, Hongoli alisema kamati yake inaishauri serikali kulipa stahiki za majenerali wastaafu kama zinavyoidhinisha kila mwaka.
Alibainisha kuwa mwaka huu wa fedha, ziliidhinishwa Sh. bilioni 3.95 kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini zilizotoka hadi Machi mwaka huu ni Sh. bilioni moja, sawa na asilimia 25.
MIKAKATI 9
Awali akiwasilisha bungeni jana hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hussein Mwinyi, alisema ulinzi na usalama wa nchi upo imara na JWTZ linaendelea kutekeleza majukumu ya ulinzi mipakani kwa weledi, umakini na hakuna matukio ya uhasama na nchi jirani.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi alisema kuwa katika kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa JWTZ katika kutekeleza majukumu yake, serikali imeweka mikakati tisa kufanikisha mpango huo.
Alisema kuwa mwaka ujao wa fedha, serikali italipatia JWTZ wataalamu, vifaa, zana bora pamoja na kutoa mafunzo kwa wanajeshi ili kuliongezea uwezo wa kiutendaji kivita.
Waziri huyo pia alisema wataboresha mazingira ya kazi, makazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma stahili na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi raia.
Alisema mkakati mwingine ni kuwapatia vijana wa kitanzania mafunzo ya uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa na stadi za kazi, kuendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa kuimarisha na kuanzisha viwanda kwa madhumuni ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.
Waziri Mwinyi alibainisha hatua nyingine itakayochukuliwa ni kuimarisha ushirikiano wa jumuiya za kimataifa, kikanda na nchi kati nyanja za kijeshi na kiulinzi.
Alisema kuwa katika kipindi hicho, serikali pia itaendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura pale inapohitajika.
Dk. Mwinyi aliutaja mkakati mwingine kuwa ni kuendesha mafunzo na mazoezi kwa jeshi la akiba na kuboresha mawasiliano salama jeshini.
Alisema JWTZ limeendelea kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa mipaka na mengine yanayotolewa kwa mujibu wa sheria kwa weledi na umakini kuhakikisha nchi inakuwa salama.
“Kuendelea kuwapo kwa migogoro na viashiria vya machafuko ya ndani katika baadhi ya nchi ambazo taifa linapakana nazo, kumesababisha ongezeko la wakimbizi na wahalifu wanaoingia nchini wakiwamo wenye silaha za moto na kuzitumia katika uhalifu,” alisema.
MGOGORO WA MALAWI
Waziri Mwinyi pia alizungumzia mgogoro wa mpaka baina ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, akibainisha kuwa bado haujapatiwa ufumbuzi.
Alisema juhudi za pamoja kati ya serikali ya Tanzania na Malawi zinaendelea chini ya usuluhishi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo kwa njia ya amani.
“Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Zambia, kuna changamoto ya ujenzi holela katika eneo la Tunduma. Ujenzi huo umefanyika hadi ndani ya eneo la Mkuza ambalo linapaswa kuwa wazi kulingana na makubaliano ya nchi na nchi,” Dk. Mwinyi alisema na kuongeza:
“Hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuendelea kuimarisha vikosi na viteule vilivyo jirani na mpaka huo, pia kuanzisha vikosi na viteule katika maeneo yenye uhitaji.”
Waziri huyo alitaja hatua nyingine katika kukabiliana na hali hiyo kuwa ni kufanyika vikao vya pamoja na wataalamu wa mamlaka zenye dhamana ya ardhi ya Tanzania na Zambia.
WANAJESHI WALIOUAWA DRC
Waziri Mwinyi pia alizungumzia kuuawa kwa wanajeshi wa Tanzania ughaibuni, akieleza kuwa Septemba, Oktoba na Desemba mwaka jana, vikosi vya Tanzania vilivyo kwenye jukumu la kulinda amani nchini DRC maeneo ya Mamondioma na Simulike, vilishambuliwa na makundi ya waasi kwa nyakati tofauti.
Alisema tukio hilo lilisababisha wanajeshi 19 kupoteza maisha na wengine 66 walijeruhiwa, lakini akasisitiza kuwa maafa yaliyotokea kwa wanajeshi hao hayakusababishwa na ukosefu wa mafunzo.
“Maofisa na askari hao walipata mafunzo ya kutosha kabla ya kwenda na waliendelea kupata mafunzo zaidi wakiwa katika eneo la operesheni,” alisema Dk. Mwinyi na kuongeza:
“Kushambuliwa kwao na kupoteza maisha ni kwa sababu waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) walifanya shambulio la kushtukiza wakiwa na nguvu kubwa. Pia maofisa na askari wetu walichelewa kupata msaada stahiki kwa wakati kutoka MONUSCO.”
Dk. Mwinyi alisema timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa (UN) imefanya uchunguzi na mapendekezo ya timu hiyo yanafanyiwa kazi na wadau mbalimbali wakiwamo UN, MONUSCO na Tanzania.
Ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri Mwinyi aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh. trilioni 1.9 kwa ajili ya wizara hiyo. Chombo hicho cha kutunga sheria kiliidhinisha bajeti ya Sh. trilioni 1.725 kwa ajili ya wizara hiyo.
Chanzo- Nipashe